• CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM CHAMA MAKINI KINACHOFANYA MAAMUZI KWA VIKAO RASMI
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA

Ni ujinga kuitumia kesi ya Mahalu kuwachonganisha Mkapa, Kikwete


Na Charles Charles
 KESI ya tuhuma za kuhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, ilifikia mwisho wiki mbili zilizopita huku yeye na mtuhumiwa mwenzake, Grace Martin wakiachiliwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo iliyofunguliwa na Jamhuri dhdi yao mwaka 2007, ilivuta hisia za wengi baada ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kusimama kizimbani na kuiambia mahakama kuwa anavyomfahamu yeye, Mahalu aliitumikia serikali kwa uadilifu, uaminifu na uchapakazi mkubwa alipokuwa mtumishi wake.

Sitaki kurejea utetezi huo wala maelezo yoyote ya upande wa Jamhuri ambayo katika shauri hilo iliwakilishwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Sitafanya  hivyo kwa sababu ninaamini kwa namna zote kuwa hukumu hiyo imetolewa kwa kuzingatia haki na misingi yote ya kisheria.

Katika hali hiyo, kwangu mimi ni ujinga mkubwa kuona kuwa tayari kuna watu wameanza kuitumia kesi hiyo kufanya uchochezi wa makusudi, ugombanishi na uchonganishi kati ya Mkapa na Rais Jakaya Kikwete, kazi inayolenga kuanzisha na kupandikiza mgogoro katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya malengo ya kisiasa ya mwaka 2015.

Nimekuwa nikieleza mara kadhaa jinsi gani Tanzania ya leo inakabiliwa na wimbi kubwa la viongozi wa kisiasa wanaoumwa ugonjwa hatari unaofahamika kitaalamu kwa jina la “uchu madaraka”, ule ambao virusi vyake hatimaye vimesambazwa hadi kwa waandishi wa habari wa baadhi ya magazeti ili nao wavieneze kwa wasomaji wao.

Hao virusi hivyo wanapandikiziwa vichwani mwao ili kuwaambukizia kifafa cha hasira, wivu na ujinga wa kutofikiri wenyewe. Wanapandikiziwa virusi vya kuamini kila uzushi, umbeya na uongo wa aina zote unaotoka kwenye vinywa vya matapeli wa kisiasa.

Fikiria kwa mfano mtu anakuja na madai eti kesi ya Mahalu imeibua uadui wa kisiasa kati ya Mkapa na Kikwete, na kwamba imeacha doa kubwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Nne. Angalia wanavyosema hadharani kama nyani kuwa kesi nyingi zinafunguliwa mahakamani ili kukomoana au kulipiziana visasi!

Yatazame madai haya ya kijinga kuwa baadhi ya kesi zimefunguliwa kutokana na shinikizo linalofanywa na baadhi ya vigogo wa CCM na serikali, kazi inayofanyika kwa kumlazimisha Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP), Elieza Feleshi huku yeye mwenyewe akiwa hataki kuzipeleka mahakamani.

Wanafanya kila wanavyoweza kutengeneza uongo wa mezani, kuumwaga hadharani na kesi ya Mahalu wameanza kuitumia kuwa moja ya silaha za kuwapandikizia umbeya watu. Hii wanaitengenezea uzushi kwamba imeibua uadui mkubwa kabisa wa kisiasa kati ya Mkapa na Kikwete ambapo sasa hawaelewani.

“Inadaiwa ndani ya kesi nyingi zilizopewa nguvu ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka zinahusishwa moja kwa moja na kundi la wanamtandao ambao kwa kiasi kikubwa, ndilo linadaiwa (kwamba) limemeza mamlaka makubwa yanayopaswa kufanywa na serikali”, unasema uzushi huo ambao unatangazwa chini ya mwavuli wa “machambuzi wa masuala ya sheria” ingawaje huo wote ni uongo, utapeli na uzandiki.

Wanafanya hivyo kwa makusudi ili kutaka kuleta mtafaruku ndani ya serikali kwa sababu wanafahamu kwamba hakuna mtandao wowote uliopo. Wanajua makundi katika vyama vya siasa yanakuwepo siku zote kunapokuwa na uchaguzi wa aina na ngazi yoyote, lakini hayo yote yanavunjika pindi unapopita isipokuwa labda katika vyama nje ya CCM.

Ndiyo maana kwa mfano katika vyama vingine, mtu yeyote asiyekuwa mwenyeji wa kanda fulani teule hivi leo hawezi kushika nafasi muhimu hasa za maamuzi ya mwisho kama kuwa Mwenyekiti wa Taifa, Katibu Mkuu au Mkurugenzi wa Fedha na Utawala hata akiwa na sifa zote anazopaswa awe nazo kwa ajili hiyo.  

Kesi iliyokuwa ikimkabili Mahalu na Grace ni shauri la kisheria sawasawa na nyingine zote zilizowahi kufunguliwa na Jamhuri tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza, ya Pili na ya Tatu dhidi ya watu wakiwa mmojammoja na hata vikundi.

Mashtaka yoyote ya madai au ya jinai yakiwa mahakamani hufuata kanuni na taratibu nzima za kisheria, hivyo mwisho wake ni lazima apatikane mshindi na kamwe hakuna sare yoyote. Ndivyo kesi ya Mahalu ilivyohitimishwa kwa upande wa utetezi kushinda, lakini wahuni wa kisiasa au kwa kuwatumia mawakala ambao ni pamoja na waandishi wa habari wanaigeuza kuwa mtaji wa kutafutia madaraka.

Wanafanya hivyo wakilenga kuwadanganya wananchi na hasa kuivuruga CCM. Wanataka kuwaaminisha kuwa kesi hiyo imewagonganisha Mkapa na Kikwete na kuwa maadui, hatua ambayo itawavunja nguvu wanachama, viongozi na wafuasi wa chama hicho na kuona sasa hakifai na kuachana nacho.

Uongo huo unafanywa kwa makusudi baada ya wahusika kuridhika bila mashaka yoyote kuwa CCM bado inaungwa mkono na wananchi wengi, hivyo hata iweje wapiga kura bado wataipa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa serikali za vitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2014, kisha itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015.

Ndiyo maana hawataki kusema ukweli kwamba kesi za kuhujumu uchumi dhidi ya vigogo waliowahi kuitumikia serikali hazikuanzia leo. Wanaficha kwa sababu wanataka kufanya utapeli, umbeya na uzushi unaolenga kuwagonganisha wana CCM wakidhani hiyo inaweza kuwa njia rahisi kwao kushinda uchaguzi ujao.

Hawasemi kwa mfano kwamba aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wa mwisho wa Serikali ya Awamu ya Pili, Nalaila Kiula alishtakiwa kwa tuhuma kama za Mahalu wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu ikiongozwa na Rais Benjamin Mkapa.

Alishtakiwa baada ya kutajwa na Tume ya Kuchunguza Rushwa iliyoundwa na Mkapa miezi michache tu baada ya kuingia kwake madarakani, ile ambayo iliongozwa na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa zamani, Jaji Joseph Warioba.

Ikiwa imevuta hisia za wengi, kesi hiyo ilimalizika kwa Kiula kuachiliwa huru, lakini kwa vile kipindi hicho hawakuwepo wambeya kama sasa, hakuna aliyedai iwe kwenye gazeti au sehemu nyingine yoyote kwamba hatua hiyo ilijenga uadui wa kisiasa kati ya Mkapa na Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Hayakutokea madai hayo kwa sababu vyama vinavyotegemea propaganda za magazeti na uzushi vilikuwa vikiongozwa na wazee wenye busara na hekima zao, lakini hivi leo vina watu waliokuwa ma-Dj wa muziki wa disko na watawa walioshindwa, wale ambao sasa ndio viongozi wake wakuu baada ya kunyoa rasta zao vichwani na kuvua majoho ya ukasisi.

Tayari baadhi yao wameanzisha mpaka vyombo vya habari vinavyofanya kazi kubwa ya kutunga na kuhubiri uzushi. Vinadandia takribani kila jambo linalofanyika na kuihusisha kwa namna moja ama nyingine serikali. Vinawadanganya wasomaji au wasikiliza wake kwa kuwalisha umbeya na uongo na mfano halisi ni kesi ya Jamhuri dhidi ya Mahalu na Grace iliyomalizika wiki mbili zilizopita.

Nimesema mapema kwamba hakuna sare katika kesi yoyote na mahali popote duniani ila ni kushinda au kushindwa peke yake. Hakuna misuli wala ujanja wowote unaotumika ili kupata ushindi isipokuwa vifungu vya sheria, vielelezo na misingi mingine, na pia hakuna mashtaka ambayo mlalamikaji huwa rais aliyepo madarakani dhidi ya mtangulizi wake.

Mathalani, kesi ya Jamhuri dhidi ya Kiula haikuandaliwa kwa namna yoyote ile na Mkapa. Haikufunguliwa ili kumwonyesha Mwinyi kwamba baadhi ya mawaziri wake walikuwa ni mafisadi.

Hata pale mshtakiwa alipokuja kuachiliwa huru mahakamani kamwe haikumanisha kwamba Mwinyi alimshinda Mkapa, na pia haukuzuka uadui wowote kati yao wenyewe wala wafuasi wao wa kisiasa na hata vinginevyo.

Kana kwamba haitoshi, wale wanaokuja na uzushi huo sasa ndio walewale wanaopiga kelele sana kuwa serikali inawalinda watuhumiwa wa ufisadi na jinai nyingine. Wamekuwa mstari wa mbele kutoa kila aina ya uongo hasa kwa wanachama wa CCM, kisha hushinikiza madai yao yatekelezwe hata kama ni dhahiri kwamba wanataka washtakiwe kwa sababu za kisiasa tu.

Ndiyo maana wamejipembua kuwa mabingwa wa kuchambua mitaji na biashara za viongozi au wabunge wa CCM peke yake, lakini hawafanyi hivyo kwa viongozi wala wabunge wa vyama vyao. Siku zote wapo radhi na tayari kuwatetea kwa nguvu zao zote, wakati wowote na mahali popote hata kama kwa kufanya hivyo wanafahamu kwamba wanatapeli watu.

Leo watuhumiwa wanapopelekwa mahakamani na kushinda kesi wanaibua madai mengine. Hii inathibitisha jinsi gani vichwa vyao vinavyofikiria majungu muda wote, halafu vinywa vyao vinanuka kila harufu ya fitina kwa serikali iliyopo madarakani.

Badala ya kuheshimu utawala wa sheria, wazandiki hao wanataka eti serikali iwe inatumia mabavu na kuingilia mihimili mingine ya dola ikiwemo mahakama, ile ambayo jukumu lake kubwa ni kutafsiri sheria zote zilizotungwa na mhimili wa bunge

Walitaka Mahalu afungwe jela ili watumie kifungo chake kuwa mtaji wao wa kisiasa, halafu walidhani angepelekwa gerezani ili waanze kuwazungukia wafadhili wao kwenda kuomba fedha wakisema ni za vuguvugu la kumtetea “mpaka kieleweke”.

Baada ya malengo yao kugonga ukuta, sasa wanatengeneza tuhuma za uongo na majungu, na pia wanataka kuitumia hukumu hiyo kuwachonganisha Mkapa na Rais Kikwete, jaribio  la kijinga ambalo hata hivyo haliwezi kuwasaidia chochote.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220, 0762 633 244 na 0782 133 996


This entry was posted in

Leave a Reply