Na Charels Charles
SIKU
moja baada ya Jeshi la Polisi Tanzania kuyasambaratisha maandamano ya kutaka kushinikiza
kuachiliwa huru kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh
Ponda Issa Ponda na wafuasi wake wanaokabiliwa na kesi mahakamani, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiliongea na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam na kuunga mkono udini, vurugu na uhalifu mwingine.
Wajumbe
wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando,
walidai kuwa serikali imeshindwa kushughulikia kwa miongo mingi madai ya
waislamu, hatua iliyochochea vurugu katika miji ya Zanzibar
na Dar es Salaam !
Marando
kwa mfano alisema serikali imewahi kuzua kuwa chama cha Civic United Front
(CUF) ni cha kiislamu, na sasa inaeneza propaganda kwamba Chadema nayo ni ya
wakristo hususan wakatoliki.
Wakizuungumza
kwa kupokezana kama walivyonukuliwa na baadhi
ya magazeti, Marando na Safari waliilaumu serikali kwa kutuma polisi kuzima
maandamano na kuwakamata watu wanaokimbia ili kukwepa wasitiwe mbaroni.
Baadhi
ya malalamiko waliyodai yanapuuzwa na serikali ni kuanzishwa kwa Mahakama ya
Kadhi Tanzania Bara, Tanzania
kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu Duniani (OIC) na kushinikiza kipengele
cha dini katika sensa ya watu na makazi.
Wakizungumzia
kutoweka kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Uamsho)
ambaye hatimaye alipochoka kujificha akajitoa mwenyewe mafichoni, Sheikh Faridi
Hadi Ahmed, viongozi hao waandamizi wa Chadema waliishangaa serikali eti kwa
kutojua alikokwenda!
“Inakuwaje
serikali ijidanganye kuwa haijui alipo na kusababisha vurugu, uchomaji moto na
kuharibu mali na hata kifo
cha polisi Saidi Abdulrahmani aliyepigwa mapanga kuhusiana na tukio hilo ? Alihoji Marando, ‘shushushu’
wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa ambaye hivi leo ni Mkuu wa Kitengo cha Intelijensia
cha Chadema.
Kwa
muda mrefu sasa nimekuwa nafuatilia kauli na matendo mbalimbali yanayofanywa na
viongozi wa Chadema wakiongozwa na gwiji la siasa za ghiliba, uzushi, uongo,
uchochezi na kila aina ya vurugu na uvunjaji wa sheria kwa makusudi lililopewa
kazi ya kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho baada ya kushindwa useja wa Kanisa
Katoliki, Dk. Wilbroad Slaa.
Wapambe
linaowaongoza katika kufanya hivyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
wa Taifa ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo jijini Dar es Salaam, John Mnyika;
Mjumbe wa Kamati Kuu na Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema na
‘vichwa maji’ wengine wa kisiasa kama Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa,
Mbunge wa Nyamagana mkoani Mwanza, Ezekiel Wenje na kadhalika.
Naweza
kusema bila ya kumung’unya maneno kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kwa
Tanzania Bara ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ndiye
kiongozi mwandamizi peke yake aliyejaliwa angalau kidogo tone la hekima,
busara, adabu na siasa za kistaarabu.
Anazungumza
kwa utafiti, tafakuri, nidhamu na hatetei uongo wala kukumbatia uzushi eti ili
mradi tu unakinufaisha chama chake hata kama
ni hatari kubwa kwa Watanzania wengine.
Ukimwondoa
Zitto peke yake, wote waliobaki wanapapasa kila kona ili kusaka mlango wa
kuwatoa. Wanafanya kila aina ya siasa chafu ikiwemo uviziaji wa matukio bila
kuangalia au kujali kitu chochote.
Ndiyo
maana kila ‘wanachogusa’ wanadhania ‘mlango wa kuwatoa’ kisiasa iwe kwa
ghiliba, uzushi, uongo, uchochezi, hadaa, umbeya ama uchonganishi na hatimaye sasa
wanashabikia au kuchekelea mpaka uhuni, vurugu, wizi, uvunjaji wa sheria kwa
makusudi na uvunjifu wa amani!
Sikutarajia
hata kidogo kuwaona wanasheria wa siku nyingi akiwemo mpaka profesa, tena ni
wanasiasa ambao ni Wajumbe wa Kamati Kuu ya chama chao wakishabikia hali hiyo
badala ya kutumia midomo yao
kuikaripia, kuisuta, kuikemea, kuilaani na sema vingine vyovyote ujuavyo.
Haiwezekani
kwa viongozi wa juu kiasi kile katika chama kinachodai kutawala nchi mwaka 2015
wakawa kama zezeta wa kisiasa.
Haiwezekani
wakaunga mkono uhuni, wizi ama uhalifu mwingine wowote unaofanywa na mtu yeyote
bila ya kujali itikadi yake ya kisiasa, dini yake, kabila lake, familia yake,
ukoo wake au eneo gani analotoka hapa nchini.
Haiwezekani
mwanasiasa wa siku nyingi kama Marando aliyewahi
hadi kuwa Mwenyekiti wa Taifa na Katibu Mkuu wa chama cha siasa hivi leo
ashabikie uozo na vurugu za kijinga.
Haiwezekani
eti kila kundi au mtu anapozuka tu asubuhi na kutaka chochote, wakati wowote na
kwa namna yoyote ile basi serikali ikubali na kutekeleza matakwa yake yote,
vilevile na bila kuangalia na hata kujali athari zake kwa taifa ama wananchi
wengine.
Haiwezekani
kwa mfano wakitokea wendawazimu wachache siku moja wakaamka asubuhi na bangi
zao vichwani, wakafunga barabara kwa maandamano, wakachoma moto majengo na
magari ya watu, kupora maduka na kufanya uhalifu mwingine washinikiza majambazi
wote waliofungwa jela waachiliwe huru eti serikali isikilizwe matakwa yao na kuyatekeleza.
Haiwezekani
hata siku moja kuwa likitokea kundi la watu au taasisi yoyote ikaleta madai ya
kutaka serikali ifute dini zote za kigeni, iruhusu matambiko kwenye ofisi zake kama Ikulu, wizarani au kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya na
gharama zote zilipwe na Halmashauri za Wilaya au Manispaa waliko kwa sababu ni
sehemu ya ibada zao basi waruhusiwe.
Haiwezekani
kwamba wakitokea watu wakataka kuwa mahakama za ngazi zote nchini ziwe pia na
ofisi za maaskofu, wachungaji, mapadri, mapasta, wainjilisti, makatekista au
viongozi wengine wa kikristu na gharama zote ziwe mikononi mwa serikali basi
wasikilizwe na hasa madai yao
hayo yakidumu kwa miongo mingi.
Haiwezekani
eti wasiposikilizwa kwa miongo hiyo basi watafute kisingizio chochote cha
kuingia barabarani na kuandamana, kufanya vurugu na kushinikiza serikali itekeleze
kwa asilimia 100 matakwa yao
yote.
Mfano
uliotolewa wa madai “ya miongo mingi” ya waislamu ya kutaka Mahakama ya Kadhi
(Tanzania Bara) hata Marando na Safari wanafahamu kuhusu undani na ukweli.
Wanaelewa kuwa tayari chombo hicho kimeshaundwa,
lakini wakorofi wachache wanaendelea kusema vinginevyo na kulazimisha mambo
yaliyopo nje ya Katiba ya nchi hii.
Mahakama
ya Kadhi ni taasisi inayowahusu waislamu na uislamu peke yake na si wananchi
wote. Haihusiani kwa namna yoyote ile na kundi jingine lolote, hivyo
haiwezekani iwe ni sehemu ya Mahakama Kuu ya Tanzania wala Mahakama ya Rufani.
Inatakiwa
iwe taasisi isiyokuwa ya kiserikali na gharama zake zote zitolewe, zisimamiwe
na kuratibu kwa kuzingatia sheria, misingi na taratibu za dini hiyo yenyewe na
siyo serikali.
Ibara
ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Toleo la
2005 inayotumika sasa inasema: “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na
ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa”
(mwisho wa kunukuu).
Hapa
maneno “isiyokuwa na dini” yana maana kwamba haifungamani na imani yoyote ile
ya kiroho, hivyo haiwezekani kuwa serikali isimamie ama kuendesha taasisi yoyote
ile ya kidini isipokuwa watu wake, kila mmoja kwa imani yake anaruhusiwa
kuabudu au kuamini dini yoyote.
Hiyo
ndiyo ibara inayoharamisha Mahakama ya Kadhi kusimamiwa, kuendeshwa na hata
kugharamiwa na serikali, badala yake kazi hizo zote zinapaswa zifanywe na
waislamu kwa kuzingatia misingi na kanuni zinazohusu uislamu.
Aidha,
ibara hiyohiyo ndiyo pia inayoharamisha kwa namna zote Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu Duniani (OIC). Ndiyo ileile iliyozuia na
kuharamisha kuwepo na dodoso la dini katika sensa ya watu na makazi kutokana na
sababu zilezile zinazozuia Mahakama ya Kadhi kusimamiwa, kuendeshwa na hata
kugharamiwa na serikali.
Mtu
ambaye anaingia mitaani kuandamana kwa vurugu, wizi, uhuni, uvunjaji wa sheria
na kuhatarisha amani ya watu wengine akishinikiza kuvunjwa kwa katiba, kisha
wakatokea wanasheria na kutetea ujinga huo hawawezi kueleweka vinginevyo ila ni
ulevi wa kisiasa, kuchanganyikiwa kimtazamo ama udhaifu wa kufikiri na kupembua
mambo ya msingi kwa nchi yao!
Kuhusu
madai eti kwamba serikali imewahi kusema CUF ni chama cha kiislamu na halafu sasa
inasema Chadema ni cha wakristo hususan wakatoliki pia nazo ni tuhuma za
kughushi, kubuni na uongo.
Ni
mkutano gani wa serikali ambako Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri,
Naibu Waziri, Mkuu wa Mkoa ama Mkuu wa Wilaya aliyasema maneno hayo na alikuwa
nani na lini kama siyo uzushi, umbeya na
uzandiki wao wenyewe midomoni mwao?
Kana
kwamba haitoshi, nawashangaa Marando na Safari kuisingizia serikali eti kwamba
ilisababisha kuzuka vurugu, uchomaji moto barabarani, wizi na uharibifu wa mali kwa
kutojua alikokuwa Kiongozi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar
(Umasho), Sheikh Faridi Hadi Ahmed!
Hivi
ni kazi ya vyombo vya dola kumlinda kila sekunde, dakika au saa ya uhai wake
utadhani Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu? Kama
anaondoka nyumbani kwake, anakwenda safari zake anapaswa aige serikali ili impe
ulinzi au amuage mkewe na watoto wake?
Aidha,
nashindwa kabisa kumwelewa mwanasheria Safari anapotaka eti mhalifu akikimbia asikamatwe.
Hivi kama akivamiwa yeye, akafanyiwa ukatili wowote unaoitwa jinai, kisha mhalifu
akakimbia hawezi kumkimbiza wala kupiga kelele zozote za kuomba msaada ili
akamatwe eti kwa sababu amekimbia?
Kwa
nini uprofesa wake wa sheria anataka kuufananisha na uprofesa wa mitishamba kama alionao Maji Marefu ama aliokuwa nao marehemu ‘Profesa’
Vulata?
Mbali
na Safari, kwa nini pia Marando anataka ajidhalilishe kiasi kile utadhani mwanasheria
wa maigizo au ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Deiwaka wa Makaburini?
Mwisho
kabisa ni je; inakuwaje Chadema waunge mkono uhuni, vurugu, wizi na uvunjifu wa
amani? Hawa ni kweli wanastahili kupewa madaraka ili walete serikali inayotetea
wezi, wahuni, wachochezi huku wakichekelea umwagaji wa damu?
Nawaomba
wananchi wote bila kujali itikadi za kisiasa kwamba kamwe wasiruhusu utawala ambao
utawaacha wakichinjwa kama kuku wa kitoweo, kuchomewa nyumba zao, maduka yao , maghala yao , misikiti yao au makanisa yao ;
halafu mhalifu eti akishakimbia inakuwa marufuku kumkimbiza ama kumtia mbaroni.
Itakuwa
marufuku kumkimbiza au kumkamata kibaka aliyepora mtaani, jambazi aliyevamia popote
na kuvunja, kuiba na hata kufanya mauaji yoyote.
Huo
ndio undani na ukweli wa Chadema uliobainishwa na Wajumbe wa Kamati Kuu ya
Chama hicho, Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari na mimi nasema “ahsanteni
sana ”.
Mungu
Ibariki Tanzania !
Mwandishi wa makala hii ni Katibu
Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu
Na. 0659 220 220 na 0762 633 244