Na Charles Charles
JUMATANO
iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania ,
Sheikh Kondo Bungo, alinukuliwa na gazeti moja la kila siku nchini, akitangaza
kufanyika kwa maandamano makubwa nchi nzima wiki hii, kushinikiza kuachiliwa huru
kwa Katibu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake waliofunguliwa
kesi mahakamani.
Wito
wa Sheikh Kondo ulikuja siku tatu tu baada ya Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari na Mabere
Nyaucho Marando, kutangaza kuyaunga mkono maandamano yote ya vurugu yaliyofanywa
na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Sheikh Ponda, Tanzania Bara, na wafuasi wa
Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu (Uamsho), kwa Zanzibar.
Aidha,
chama cha Civic United Front (CUF) kupitia kwa Mwenyekiti wa Taifa, Profesa
Ibrahim Haruna Lipumba nacho kilijitokeza hadharani, siku moja baada ya kauli
ya Sheikh Kondo, kutaka Sheikh Ponda na wafuasi wake walioshtakiwa Oktoba 18, waachiliwe
huru na kusema kuwa kitendo cha serikali cha kupeleka Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) kutaka kupambana na waandamanaji “ni cha aibu na
kinasikitisha”.
Tayari
Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT), limeomba radhi
kwa waislamu wote nchini walioguswa kwa namna moja ama nyingine na kukojolewa
kwa Kitabu Kitukufu cha Kur’ani, kitendo kilichofanywa Oktoba 12, mwaka huu, na
mtoto wa Shule ya Sekondari ya Nzasa jijini Dar es Salaam.
Kufuatia
maandamano ya vurugu yaliyofanywa na watu wanaoaminika kuwa ni waislamu, kwanza
huko Mbagala, Oktoba 12, kupinga kudhalilishwa kwa kitabu hicho cha dini yao na kutaka wakabidhiwe
mtoto huyo ili wamchinje hadharani.
Siku
chache baadaye ilipofika Oktoba 20, wafuasi wa Sheikh Ponda anayekabiliwa na
kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, nao
waliandamana, kushinikiza aachiliwe huru yeye na wafuasi wake anaoshtakiwa nao
kwa tuhuma nyingine za jinai. Hapo ndipo serikali ikatuma takribani kombania tatu
za JWTZ ili zisaidiane na askari wa Jeshi la Polisi kukabiliana na wafanya fujo
hao.
Kesho
yake, serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel John Nchimbi
ndipo ikasema kwamba walioshiriki katika vitendo hivyo vyote ni wahuni tu.
Alikuwa
akimaanisha sababu za kuandamana kwao huku wakifanya vurugu, kuyavamia makanisa
na kuyavunja, wakaiba mikate ya meza ya Bwana na divai zake, wakachoma Biblia,
kukojolea madhabahu, kuiba kwenye maduka ya watu, kusababisha kufungwa kwa
shughuli zote katikati ya jiji na uhalifu mwingine kwamba hakuhusiani chochote
na msingi wowote ule wa kidini.
Alimaanisha
kwamba huo ni uhalifu kama mwingine wowote ule
wa jinai. Hautokani na agizo wala kitabu cha dini yoyote, hivyo hawawezi kusingizia
kwamba walifanya hivyo ili kutetea haki, hadhi wala sheria za dini yoyote bali
ni wahuni wanaotaka kuutumia uislamu kuwa kichaka cha kufichia uhalifu wao.
Pamoja
na ukweli huo wote, kauli hiyo ya Nchimbi bado imeonyesha kutokubaliwa na PCT
kupitia taarifa yake iliyosomwa kwa waandishi wa habari na mmoja kati wa
wajumbe wake, Dk. Mgulu Kilimba.
“Kauli
hiyo inamaanisha kuwa serikali haiamini kuwa waliohusika na uvunjaji wa
makanisa, kuchoma (moto) Biblia, kubomoa na kukojolea madhabahu, kunywa na kula
mikate ya meza ya Bwana na hatimaye kuwapiga watumishi wa Mungu ni wanaharakati
wa kidini”, inasema taarifa hiyo.
Nimefuatilia
kwa muda mrefu sakata hili zima lilipoanza kwa mtoto yule kuikojolea Kur’ani na
kusababisha maandamano yale ya ghasia, uporaji ukiwemo wa kutumia nguvu,
uvunjaji wa makanisa, uchomaji moto Biblia, kukojolea madhabahu kanisani mpaka
maandamano ya pili yaliyodhibitiwa kikamilifu, katikati ya jiji hilo la Dar es Salaam.
Nimeziangalia
hoja na madai yanayotolewa na watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa kama akina
Profesa Abdallah Safari, Mabere Marando, Profesa Ibrahim Lipumba, Sheikh Kondo
Bungo na hatimaye PCT mbali na ubishi unaotokea mitaani na sehemu nyingine hasa
zenye mikusanyiko ya watu wa kada na fani tofauti.
Wengi
kati yao hawakubaliani moja kwa moja na
maandamano yote yaliyofanywa kuanzia ya Mbagala hadi ya Oktoba 17 huko Zanzibar na hata yaliyodhibitiwa na polisi katika mitaa ya
Kariakoo, Magomeni, Mnazi Mmoja na maeneo mengine jijini Dar es Salaam , siku mbili baadaye.
Hawakubaliani
nayo kwa sababu yanaonekana kwamba yalifanyika kwa kupangwa na hivyo madai
yaliyotolewa na wahusika ambayo yamekuja kushadidiwa na watu kama
akina Safari, Marando, Lipumba na Sheikh Kondo ni visingizio vinavyolenga
kuficha malengo halisi.
Pamoja
na kutofungamana na upande wowote kati ya zote zinazovutana, lakini nakubaliana
na wale wanaolaani mikakati na kauli zote zinazounga mkono uovu huo. Nakubaliana
nao maana hakuna ubishi kwamba hata kwa sheria zote duniani, mtu yeyote mwenye
umri wa chini ya miaka 18 bado ni mtoto.
Anachukuliwa
kuwa hawezi kuchanganua jema au jambo lolote ambalo ni baya kwa vile hajui
lolote wala chochote maana ni mtoto na hivyo akili zake pia ni changa.
Ndivyo
ilivyokuwa kwa mtoto huyo wa Mbagala aliyekojolea Kur’ani. Hakufanya hivyo kwa
makusudia ama nia yoyote ile kwa waislamu na uislamu kama
dini. Ndiyo maana pia inaelezwa kuwa alikikojolea kitabu hicho ili kuona kama vitisho alivyokuwa akitishiwa na mwenzake vina
ukweli au vilikuwa hadithi za alinacha.
Kama
inavyofahamika dunia nzima, hakuna watu wanaopenda sana
kujaribu kitu chochote kama watoto. Ndiyo
maana wataalamu wanaeleza wazi kuwa mtoto ndiye binadamu ambaye ana uwezo
mkubwa zaidi wa kukariri mambo au kufanya majaribio mpaka aridhike.
Anapenda
kuthibitisha kila jambo analosikia, kuambiwa au kuhadithiwa kwa kutaka kuona
kwa macho yake mwenyewe, kushika au kugusa kwa mikono yake, kuonja kwa ulimi
wake, kuongelesha kwa kinywa chake na kadhalika. Hawezi kuambiwa kitu na hasa
anachodhani kuwa kinasisimua sana ,
kushangaza au kuringishia halafu akaitikia mdomoni kwa urahisi na kuishia hapo.
Ni
lazima asikilize kwa makini yake yote, abishane sana , aulize maswali, adadisi takribani kila
kipengele au ufafanuzi anaopewa na hata vinginevyo.
Ndivyo
ilivyokuwa pia kwa mtoto aliyekojolea Kur’ani ambapo kuna watu wanadai kuwa aliambiwa
kama angefanya hivyo angegeuka chatu palepale,
mbuzi ama angekumbwa na kichaa cha akili papo hapo.
Kwa
vile hakuamini vitisho hivyo na kusema haiwezekani huku mwenzake akisisitiza kuwa
ni kweli, mtoto huyo aliamua akate mzizi wa fitina kwa kuiweka chini,
akaikojolea na kisha akabaki ni binadamu yuleyule, vilevile na palepale wala
hakugeuka chatu, mbuzi au kupata wendawazimu wa akili na hata vinginevyo.
Siyasemi
haya kwa kuangalia jina langu kuwa ni mkristo kwa sababu kama
ni dini ninatoka kwenye familia ya kikristu na kiislamu. Wakati baba yangu ni
mkristu, marehemu mama yangu mzazi na marehemu dada yangu walikuwa waislamu na
mimi pia nilianzia katika dini hiyo kabla sijaamua rasmi kufuata imani ya baba.
Hadi
hivi leo kwa mfano ukienda nilipokulia pale Temeke Mikoroshini, Dar es Salaam, au
kijijini kwetu na katika ukoo wote wa mama unitafute kwa kutumia jina hili kuna
wengine watasema hawanifahamu.
Hiyo
ni kwa sababu wamezoea jina lile jingine nililokua nalo, lakini hatimaye
likayeyuka polepole na kutoweka miongoni mwao. Wakaingiwa na hili la pili
walilokuja kulifahamu rasmi nilipokuwa nasoma shule, lakini lilishika kasi
zaidi nilipoacha jeshi katika JWTZ na kuanza kazi hii ya uandishi wa habari
magazetini.
Najiuliza
pia kuhusu madai kuwa mtoto yule alitumwa na baadhi ya watu amdanganye mwenzake
kwamba kama angeikojolea Kur’ani angegeuka
chatu, mbuzi ama angepata wendawazimu papo hapo.
Walitaka
wafanye hivyo ili kukidhi matakwa yao
ya kisiasa au ya kiuchumi ikiwemo kuiba, kuvunja makanisa na kuwapiga watumishi
wake, kuchoma moto Biblia na kufanya uhalifu mwingine.
Najiuliza
kama kweli ni mpango uliosukwa na kundi la wahalifu wa kawaida mitaani, lakini
ili kuvichanganya vyombo vya dola wakamtumia mtoto huyo wa kiislamu amshawishi kwa
kutumia vitisho mtoto wa kikristu ili ashawishike kirahisi kuikojolea Kur’ani,
hatua ambayo ingewapa nafasi na sababu za kuanzishia vurugu na kukidhi matakwa
yao yote.
Walijua
kitendo hicho kingewachukiza waislamu katika upande wa kwanza, na pia walijua wasingeweza
kukivumilia, hivyo wangeutumia mwanya huo kama kisingizio cha kuanzishia vurugu
ili kutimiza matakwa yao
yakiwemo yaliyotajwa na viongozi wa PCT wiki iliyopita.
Kama
ni kweli kuwa kosa lile lilifanywa na mtoto yule ili kuudhalilisha uislamu, kwa
nini wakristu hawakuandamana popote, wakafanya ghasia, wakavunja misikiti,
kuchoma moto Kur’ani, kukojolea kibra misikitini wala kuwapiga masheikh au
maimamu ili kulipa kisasi cha uhalifu waliofanyiwa kule Mbagala?
Au,
nani aliyefanya kosa kubwa zaidi kati ya mtoto aliyekojolea Kur’ani bila kujua kuwa
ni kosa kwa kuzingatia umri wake na watu wazima waliovamia makanisa na
kuyavunjavunja, wakaiba divai na mikate ya meza ya Bwana, kuzichoma moto Biblia,
kukojolea madhabahu ya kuongozea ibada au kuwapiga watumishi wake na kadhalika?
Hadi
hapo kwa nini nisiamini kuwa hayo yaliyofanywa au yanayofanywa ama kuchochewa
na viongozi kama akina Profesa Abdallah
Safari, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, Mabere Nyaucho Marando, Sheikh Kondo Bungo
na wengineo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mzito wa siri walionao dhidi ya
Serikali ya Awamu ya Nne?
Kwa
nini nisiamini kuwa wanafanya hivyo ili kutimiza kilichosemwa na baadhi ya
vyama vya siasa pindi tu baada ya kushindwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na
madiwani wa mwaka 2010 kwamba watahakikisha Tanzania haitawaliki katika kipindi
hiki cha kuelekea mwaka 2015?
Mwandishi wa makala hii ni Katibu
Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu
Na. 0659 220 220 na 0762 633 244