Na Charles Charles
KATIKA
hali isiyokuwa ya kawaida, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Dk. Wilbroad Slaa aliwafanyia tafrija maalum ikiwemo kuwaitia
waandishi wa habari, mabinti wawili wa kaka wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira walipokwenda kuchukua kadi za chama
chake.
Tukio
hilo ambalo lilitokea Septemba 29, lilifanyika
Makao Makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam
ambapo Dk. Slaa aliwatumia kama mtaji wa
kisiasa, akiwataka Watanzania wengine pia waachane na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
“ili kuleta mabadiliko” nchini.
Wanawake
hao ni Lilian na Esther George Wassira na katika hotuba yake kwao, Dk. Slaa
alimshutumu baba yao
mdogo kwamba ni “kinara wa kuuaminisha umma kuwa wanaodai hali bora ya maisha
kwa Watanzania ni wenye vurugu”, lakini hafahamu endapo “maisha yakiboreka hata
wengine katika familia yake (mwenyewe nao) watayafurahia”.
Sitaki
niamini kuwa Dk. Slaa kama msomi wa falsafa ya teolojia, mbunge wa zamani,
mgombea urais aliyeshindwa, Katibu Mkuu wa chama cha siasa kinachojipa hadhi ya
upinzani mkuu kwa serikali na padri wa zamani kumbe ana upeo mfupi kiasi hicho!
Sikutarajia
kama angewaona wanawake hao ni muhimu zaidi kuliko wanachama na viongozi
wengine wa Chadema akiwemo yeye, wale ambao kila mmoja alihamia katika chama
hicho kwa muda wake na sababu anazozijua mwenyewe.
Anawaona
muhimu kuliko Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Tanzania Bara), Said Amour Arfi
aliyetokea CCM mwaka 2005; Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Saidi Issa Mzee;
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Anthony Komu na Mkuu wa Kitengo cha Intelijensia,
Mabere Nyaucho Marando waliohamia huko wakitokea NCCR – Mageuzi; Mkurugenzi wa
Kampeni na Uchaguzi, Msafiri Abdulrahman bin Salim wa Mtemelwa aliyetoka Chama
Cha Wananchi (CUF) na kadhalika!
Ibara
ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Toleo la
2005 inasema “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa,
isiyokuwa na dini na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa”.
Katika
hali hiyo, Mtanzania yeyote asiyepungua miaka 18 ana haki ya kujiunga na chama
chochote kile cha siasa, hivyo inashangaza kumuona Dk. Slaa akiingia
wendawazimu baada ya wanawake hao wawili kujiunga Chadema.
Nashangaa
kwa sababu hawana historia wala rekodi yenye tija kwa chama chochote kile cha
siasa, na pia hakuna kumbukumbu inayoonyesha kwamba walifanya jambo kubwa
lolote na mahali popote iwe nyumbani, shuleni au chuoni na hivyo kwenda kwao
Chadema ni hatua ambayo itakiletea chama hicho faida ya maana kisiasa dhidi ya
vyama vingine.
Kama
alivyosema Waziri Stephen Wassira kesho yake alipokutana na waandishi wa habari
mjini Bunda mkoani Mara, Lilian na Esther ni akina mama wa nyumbani na
wafanyakazi wa kawaida wakiwa wanasheria, hivyo hakuna faida yoyote kwao
kuingia Chadema wala pengo lolote waliloacha katika familia ama ukoo wao kwa
hatua yao hiyo.
Lakini
kwa sababu hakuna rekodi hiyo, nalazimika kuamini kwamba Dk. Slaa na Chadema
yake wanataka kuwafanya kuwa mtaji wa kisiasa siyo kwa kupitia majina yao kama Lilian na Esther George isipokuwa baba yao mdogo, Stephen Wassira.
Wanataka
kuwadanganya Watanzania kuwa ni watoto wake halisi na mkewe, ukweli ulioanza kuonekana
wakati Katibu Mkuu huyo wa Chadema alipoita waandishi wa habari na kufanya
tafrija ya kuwapokea, wakapigwa picha na kutangazwa kwenye televisheni pamoja na
magazeti kwamba wanatoka familia ya waziri huyo, kiongozi ambaye pia ni Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
“Ndugu
yangu Wassira amekuwa kinara wa kuuaminisha umma kuwa wanaodai hali bora ya
maisha kwa Watanzania ni wenye vurugu pasipo kujua maisha yakiboreka hata
wengine katika familia yake mwenyewe watanufaika”, alisema ili kuonyesha uongo
wake kwamba wanawake hao “wamekiasi chama cha baba yao ingawa ni waziri” na kisha wakakimbilia
Chadema.
Anataka
kuwadanganya Watanzania kuwa chama hicho kina sera nzuri, kinatetea wananchi na
kupigania maisha bora kwa wote na ndiyo maana sasa kinakimbiliwa hadi na watoto
wa viongozi waandamizi wa CCM na serikali yake.
Aliita
waandishi wa habari na kuwafanyia tafrija maalum siyo kwa sababu anawapenda
sana au wana kitu cha ziada kuliko Said Amour Arfi, Anthony Komu, Msafiri
Mtemelwa, Mabere Marando; Mkurugenzi wa Sera na Utafiti, Mwita Waitara; Mkurugenzi
wa Organaizesheni, Benson Kigaila na hata Wajumbe wa Kamati Kuu akina Profesa
Abdallah Safari na Profesa Mwesiga Baregu ambao pia walikwenda Chadema
wakitokea vyama vingine.
Alilenga
kuwafanya akina mama hao kwamba ni muhimu kuliko jopo hilo
lote na ndiyo maana hakuna aliyepewa mapokezi hayo maalum kama wao, hivyo kwenda
kwao Chadema kutakifanya chama hicho kiwe juu zaidi kisiasa kushinda wakati
wote mwingine kabla yao .
Hata
hivyo, kamwe sioni faida yoyote ya kisiasa kwa Chadema kutokana na hatua yao hiyo zaidi ya kuongeza
orodha ya wanachama wanawake, na pia hakuna hasara na hata pengo lolote itakalopata
CCM endapo wamewahi kuwa wanachama wake ama familia ya Waziri Stephen Wassira
ambako kwanza hawatoki.
Mwaka
1995, mtoto wa kiume wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
Kapteni Makongoro Kambarage Nyerere aliingia NCCR – Mageuzi ambako aligombea
ubunge wa Arusha Mjini na kushinda, lakini CCM haikuyumba wala kutikisika kwa
namna yoyote ile eti kwa sababu aliihama na kujiunga na upinzani.
Alidumu
katika chama hicho kwa miaka takribani sita na kurejea CCM, hatua ambayo hata
Waziri Wassira naye amewahi kuifanya alipohamia katika chama hicho mwaka uleule
wa 1995 pamoja na Makongoro, lakini akarejea alipogundua kuwa upinzani ni kama jukwaa la ‘ze komedi’.
Katika
hali hiyo, hata watoto hao wa kaka yake waziri huyo huenda wakaondoka Chadema
na kuingia chama kingine, kile ambacho kinaweza kuwa CCM ama vinginevyo, lakini
hata iweje hakuna faida yoyote itakayopatikana ya kwenda kwao huko.
Hawawezi
kufananishwa kwa namna yoyote ile kisiasa na watu kama Profesa Abdallah Safari,
Profesa Mwesiga Baregu, Said Amour Arfi, Saidi Issa Mzee, Mabere Nyaucho Marando,
Msafiri Mtemelwa, Mwita Mwikwabe Waitara, Benson Kigaila, Anthony Komu wala Mkurugenzi
wa Idara ya Ulinzi ya Chadema ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Bukoba Mjini
kupitia CUF, Wilfred Lwakatare.
Hawawezi
kuwa lolote kisiasa kuliko viongozi hao akiwemo mbunge wa sasa wa jimbo la
Kigoma Kusini (NCCR – Mageuzi), David Kafulila aliyefananishwa na sisimizi kwa
kauli iliyotolewa na Dk. Slaa mwenyewe wa waandishi wa habari mwaka 2009.
Alikashfiwa
kwa maneno yote ‘machafu’, kejeli na dharau kwa sababu tu alimuunga mkono Mbunge
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe wakati wa kinyang’anyiro cha kuwania
nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema.
Alionekana
hatari kwa sababu tu alikuwa Meneja wa Kampeni za Zitto ambaye naye alishinikizwa
ajiuzulu katika mbio hizo ili amuache Freeman Mbowe awe mgombea pekee, mfumo ambao
haupo katika chama hicho bali uliletwa ili kukidhi matakwa ya ukabila, udini na
ukanda.
Siwadharau
wala kuwakejeli wanawake hao kwa hatua yao hiyo
ya kwenda Chadema, lakini sikubaliani na juhudi za kutumia nafasi ya baba yao mdogo serikalini kutaka
kuwapandisha chati ili waonekane muhimu, na pia hakuna jambo lolote
litakaloshindikana kufanyika katika CCM eti kwa vile mabinti hao sasa hawapo.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu
Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu
Na. 0659 220 220 na 0762 633 244