Na Charles Charles
MJANE
wa mmoja kati ya wafuasi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
waliouawa wakati wa maandamano ya vurugu, ghasia na kinyume cha sheria mjini
Arusha hapo Januari 5, mwaka jana, Asia Omar, amekishutumu chama hicho kwa ‘kutafuna’
fedha za rambirambi zilizochangwa kwa ajili marehemu mumewe, Ismail Omar.
Asia
ambaye aliachiwa watoto wadogo wawili na mumewe, alifichua siri hiyo alipokuwa
akiongea kwenye mkutano wa chama cha Civic United Front (CUF), uliofanyika hivi
karibuni katika Uwanja wa Levolosi mjini humo na kusema hadi sasa, viongozi wa
Chadema bado hawajamkabidhi fedha hizo ambazo walichangisha kwenye Uwanja wa
NMC Januari 6, mwaka jana, wakati wa kuaga mwili wa marehemu mumewe.
“Nimekuja
hapa leo kuelezea machungu yangu. Nasikitika kwamba Chadema mbali na
kuchangisha fedha za rambirambi za marehemu mume wangu, hadi leo sijaiona hata
senti tano”, alisema huku akiangua kilio hadharani.
Alizitaja
fedha alizopata tangu wakati huo hadi sasa kuwa shilingi milioni tano
zilizotolewa na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustafa Sabodo, lakini
Chadema iliyotangaza kuiangalia familia yake baada ya mumewe kuuawa kwenye
maandamano yake imemsusa na kumdhulumu haki yake.
Kutokana
na kilio hicho, viongozi wa CUF mkutanoni walifanya harambee iliyokusanya kiasi
cha shilingi 500,000 taslimu na kumkabidhi papo hapo.
Siku
chache baadaye, Itika Mwangosi ambaye ni mjane wa aliyekuwa mtangazaji wa Kituo
cha Televisheni cha Channel Ten katika mkoa wa Iringa, Daud Mwangosi naye
aliibuka na kuwaomba waandishi wa habari wamsaidie kufuatilia rambirambi ya
marehemu mumewe aliyoahidiwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa.
Alisema
kuwa tokea padri huyo wa zamani atangaze kumlipia ada mtoto wa kwanza wa
marehemu Mwangosi anayeitwa Nehemiah, yule ambaye jana, Jumatatu ameanza kufanya
mitihani ya mwisho ya kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya
Malangali iliyopo wilayani Mufindi, Iringa – palepale aliposoma baba yake mzazi
– hakuna chochote alichopewa.
Akizungumza
wakati wa maziko ya marehemu Mwangosi yaliyofanyika Septemba 3 huko Rungwe
katika mkoa wa Mbeya, Dk. Slaa aliyeanza jaribio la kutaka kuuteka msiba huo
tokea Iringa, alisema amezungumza na mdau wake ambaye aliahidi kubeba jukumu
zima la kumsomesha Nehemiah kuanzia sasa hadi pale atakapoishia kielimu.
Lakini
tokea kipindi hicho, Itika amesema hakuna mawasiliano yoyote yaliyofanywa kwake
na Dk. Slaa, lakini akasema kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Asiye na Wizara
Maalum) na Mbunge wa Rungwe Mashariki (CCM), Profesa Mark Mwandosya ambaye pia
aliahidi kusimamia elimu ya kila mtoto wa familia hiyo sawa na kama baba yao
mzazi angekuwa hai ndiye anayepatikana.
Mwandosya
ambaye aliiwakilisha serikali katika maziko hayo, alisema atafanya hivyo kwa sababu
marehemu alikuwa ni ndugu na jirani yake huko Rungwe, hivyo watoto aliowaacha
ni sehemu ya familia yake.
“Nina
mawasiliano na Profesa Mark Mwandosya”, anasema mjane huyo wa marehemu na
kuongeza: “Yeye ameniambia nitakapokuwa tayari nimjulishe ili atume fedha
kwenye akaunti ya shule, lakini sina mawasiliano na Dk. Slaa”.
Hiyo
ndiyo sura “ya ndani” aliyonayo Dk. Slaa na viongozi wenzake wa Chadema. Kama ilivyoandikwa na gazeti moja litolewalo kila siku
nchini, Ijumaa iliyopita, utamaduni mpya wa siasa za misibani unaoendana na
mauaji yanayotokana na ukaidi wa wanasiasa kwa Jeshi la Polisi, hatimaye umeanza
kukiumbua chama hicho kwa “kushindwa kutekeleza ahadi ndogondogo tu za kutoa
rambirambi kinazowaahidi wafiwa”.
Kimekuwa
na ujasiri wa kutotii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuvunja kwa
makusudi sheria na kuendesha siasa za vurugu, ghasia na kila aina ya ubabe unaosababisha
kuzuka kwa mauaji ya raia wasiohusika na chochote ambao hadi sasa idadi yao
imefikia sita.
Watatu
walipoteza maisha yao
kwenye maandamano haramu mjini Arusha, Januari 5, mwaka jana, mmoja akauawa na
vijana wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa chama hicho kilipofanya mkutano wa
hadhara wilayani Iramba, Singida, Julai 14, mwaka huu.
Mwingine
aliyeingia katika orodha hiyo, Ali Zona, aliuawa katika maandamano mengine
yaliyofanywa kinyume cha sheria eneo la Msamvu mjini Morogoro mwishoni mwa
mwezi Agosti, mwaka huu pia.
Idadi
hiyo inakamilishwa na Daud Mwangosi aliyeuawa katika kijiji cha Nyololo, wilaya
ya Mufindi, Iringa, Septemba 2. Mauaji hayo yalitokea wakati askari wa Kikosi
cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi Tanzania (PT), wakijaribu kuuvunja
mkutano wa hadhara wa Chadema uliokuwa ukifanyika kinyume cha sheria.
Katika
kipindi hicho, mikutano yote ya kisiasa nchini isipokuwa ya kampeni za uchaguzi
mdogo wa kiti cha uwakilisha katika jimbo la Bububu huko Zanzibar , ilikuwa imepigwa marufuku ili
kupisha sensa ya watu na makazi.
Mara
nyingi nimekuwa nikionyesha kiasi gani viongozi wa Chadema walivyo waongo na kuwaonya
Watanzania, kwamba waepuke kuamini ghiliba na siasa zenye malengo haramu kwa
taifa lao.
Viongozi
wa Chadema kutoka wa kitaifa, mikoa, wilaya, majimbo, kata hadi vijiji na mitaa
wamekuwa wakijifanya wasamaria na watu waliojazwa roho mtakatifu, hivyo mara
zote yanapofanyika mauaji yanayosababishwa na chama hicho chenyewe wanatoa
kauli pamoja na ahadi za kuvutia ili kuwadanganya Watanzania.
Kila
mahali wanapofanya vurugu na ghasia zinazosababisha umwagaji wa damu hujitokeza
hadharani na kuishutumu serikali kwamba “inaua watu ili kuilinda CCM”, kisha
wanaahidi kufanya kila wanavyoweza kuzisaidia familia za marehemu ili “kuzifuta
machozi”.
Wanaahidi
kuzisaidia kifedha, kuzisomeshea watoto hasa walioachwa na baba zao wazazi au
walezi wao, lakini kwa kawaida hufanya hivyo wakilenga kupata wanachama na
wafuasi wa chama chao. Ndiyo maana wanafanya hivyo hadharani badala ya kuongea
faragha na wafiwa ili kujua undani halisi wa matatizo yatakayowakabili.
Kama
inavyosema Biblia Takatifu ambayo Dk. Slaa mwenyewe aliyewahi kuwa Padri wa
Kanisa Katoliki anaifahamu vyema hata kama alishindwa
kuitumikia, mtu anapotoa msaada hapaswi kufanya hivyo hadharani isipokuwa iwe
kwa siri baina yake na aliyemsaidia katika hali yoyote.
Kinasema
kitabu hicho kwamba kinachotolewa na mkono wa kulia “hata mkono wa kushoto
usijue”, hivyo inashangaza kuona kasisi huyo wa zamani anashindwa kukiheshimu
wakati alipaswa aonyeshe mfano kwa wenzake.
Badala
ya kuheshimu maandiko hayo matakatifu, Dk. Slaa amekuwa kinara wa kupenda
kujionyesha ili kutafuta sifa na kuzidi kuwaghilibu akili Watanzania, halafu
kibaya zaidi ni pale anaposhindwa kutekeleza ahadi zote anazotoa na kuwa muongo
aliyepitiliza.
Najiuliza
mengi kuhusiana na suala hilo , moja kati yake ni
kama chama hicho kinavunja sheria kwa makusudi
kwa kuitisha mikutano kinyume cha sheria, kisha inapozuiliwa na vyombo
vinavyohusika hufanya vurugu na kulilazimisha Jeshi la Polisi kuingilia kati.
Katika
kufanya hivyo, yapo maeneo ambako hutokea bahati mbaya kuwa baadhi ya watu wasio
na hatia yoyote hupoteza maisha yao kama wale waliouawa Arusha, mwaka jana.
Wanakuwa
hawana hatia kwa sababu wanapandikiziwa uzushi, uongo, hasira, fitina pamoja na
kila aina ya ukatili na kuwa wendawazimu vichwani. Wakifikia hali hiyo ndipo hujitolea
mhanga kupambana na polisi, kuwapiga watu wasiotaka kuungana nao katika
maandamano yao , kupora mali zao,
kuchoma moto magari na majengo mbalimbali yakiwemo ya biashara mbali na kufanya
uharibifu mwingine mkubwa.
Waliokuwa
Arusha, mwaka jana, watakumbuka jinsi waandamanaji waliolishwa sumu ya chuki na
hasira walivyokuwa ‘wamechanganyikiwa’ akilini, wakapita barabarani huku
wakirusha mawe kwa watu wasiotaka kuandamana, wakayachoma moto baadhi ya maduka
na kutaka kuliteketeza kwa namna hiyo pia jengo la makao makuu ya CCM la mkoa
huo.
Wakiwa
katika hali hiyo ya uendawazimu uliopitiliza, waandamanaji hao waliochochewa na
viongozi kama Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema,
Freeman Mbowe na Dk. Slaa walijaribu pia kufanya uhalifu mwingine mkubwa
kupindukia.
Walikwenda
huku wakiimba nyimbo za “pepole’s power” na kujaribu kuteka Makao Makuu ya
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, jaribio ambalo kama wangelifanikisha, jambo kubwa
la kwanza lingekuwa ni kuvamia ghala la silaha na kuziiba zote, kisha wangewaachilia
huru watuhumiwa mbalimbali wa uhalifu ukiwemo wizi wa kawaida, ujambazi wa
kutumia nguvu na kadhalika na kuhitimisha kazi hiyo kwa kuliteketeza kwa moto
jengo hilo lisiwepo tena.
Hapo
jiji la Arusha na vitongoji vyake lingegeuka kuwa uwanja wa uporaji, ujambazi
na mauaji yakiwemo ya kikatili na kila aina ya uhalifu. Ndiyo maana ilibidi
polisi wawadhibiti kwa kuwarushia risasi za moto baada ya kutotishika na zile
zilipopigwa kuelekea hewani ili watawanyike.
Ilikuwa
wakati huo ndipo watatu kati yao akiwemo Ismail Omar walipopoteza maisha yao
huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, hatua iliyotoa mwanya kwa Chadema kuwachangisha
fedha wananchi kwenye Viwanja vya NMC, kesho yake na kuwadanganya wafiwa
akiwemo Asia kuwa wangepewa kama rambirambi lakini hadi leo, mwaka mzima na
miezi tisa baadaye bado hawajapata hata senti tano!
Bahati
mbaya kijana aliyeuawa katika kijiji cha Ndago, wilaya ya Iramba mkoani Singida
alikuwa ni kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), hivyo
isingewezekana kwenda kuwadanganya wazazi wake kwa namna yoyote. Ilikuwa vigumu
kwa sababu walijua kuwa ndugu zake hawawezi ‘kudanganyiwa pipi’ na kujiunga
Chadema.
Lakini
alipouawa mtu mwingine kule Morogoro, viongozi wa Chadema walijaribu kuuteka
msiba wake ili uwe wao, wakataka wauchukue na kuusimamia kwa kila kitu na hatua
zake zote kuanzia hospitali ulikopelekwa mwili wake hadi nyumbani kwao huko
Tanga, juhudi ambazo hata hivyo ziligonga mwamba.
Ndiyo
maana haikuwa ajabu siku chache baadaye kumuona Dk. Slaa akiongoza vurugu
nyingine kubwa huko Iringa, zile ambazo hatimaye zilisababisha kifo cha
Mwangosi.
Akataka
pia kuuteka msiba ule ili uwe wa Chadema na siyo wa familia ya marehemu kutoka
nyumbani kwake, Kihesa Kilolo katika mji wa Iringa hadi kwenye maziko yake huko
Rungwe, mkoa wa Mbeya, lakini juhudi hizo nazo zikadhibitiwa na Klabu ya
Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Iringa (IPC) katika sehemu hizo zote.
Hapo
ndipo akamwahidi mjane wa marehemu, Itika kuwa angemsomeshea mtoto wake,
Nehemiah anayesoma Shule ya Sekondari ya Malangali, lakini kama
alivyomdanganya Asia Omar kule Arusha, yeye pia ameshindwa kumpa chochote kwa
sababu alikuwa akitaka sifa na siyo vinginevyo.
Alikuwa
akitaka umaarufu wa kisiasa kwake binafsi kama
Dk. Slaa. Alikuwa akikihangaikia chama chake ili kipate wanachahama zaidi.
Alikuwa akiendeleza mfumo wake wa kutumia misiba kusaka mamlaka mwaka 2015
maana ameahidi kuwa Chadema ni lazima ishinde na kutinga Ikulu, hivyo anahofia
kwamba ikishindwa naye atakuwa moja kwa moja amekwisha kisiasa.
Lakini
swali kubwa la kujiuliza hapa ni je, kama
chama hicho kinaahidi uongo hadi kwa marehemu waliokufa katika vurugu zake chenyewe
kuwa kitawapa rambirambi wake zao, kuwasomeshea watoto wao na kisha ‘kinaingia
mitini’, nani aliye hai ambaye kitaogopa kumdanganya ili kitawale?
Mwandishi wa makala hii ni Katibu
Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu
Na. 0569 220 220 na 0762 633 244