Na Charles Charles
AKIONGOZA
misa katika Kanisa Katoliki la Manzese jijini Dar es Salaam , Jumapili iliyopita, Padri
Baptiste Mapunda “alikemea tabia ya kupeana uongozi ndani ya familia moja”
akidai itakwamisha utendaji wenye tija na maendeleo.
Mapunda
ambaye ameondokea kuwa ni “padri mwanasiasa wa kambi ya upinzani nchini”,
alisema hali hiyo inaongeza pengo kati ya matajiri na masikini, kisha akawashutumu
viongozi wa kisiasa akidai wameua Azimio la Arusha alilodai lilianzishwa na
Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na kuligeuza kuwa “azimio la wala
rushwa na ufisadi”.
Alimfananisha
Rais huyo wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mtume Musa akisema
alitumia hekima na busara, kuwaondoa Watanzania katika ukoloni bila ya kutumia silaha,
na kwamba wakati wote wa utawala wake hapakuwepo migomo ya walimu, madaktari au
kuuawa kwa mwandishi wa habari.
“Jambo
la msingi tuhakikishe rais anapunguziwa madaraka na matumizi ya vyombo vya dola
yasiwepo katika siasa, viongozi wengi hawakuchaguliwa kwa haki na ndiyo maana
taifa limekuwa na majanga makubwa”, alisema kama
alivyonukuliwa na gazeti moja la kila siku nchini, Jumatatu wiki hii.
Nimewahi
kukorofishana hadharani na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Meja Jenerali
Saidi Kalembo nikimtetea Padri Mapunda alipopigwa marufuku asiongoze ibada
yoyote mkoani humo mwaka 2003, zuio alilopewa kwa sababu alikuwa akihubiri
siasa za uchochezi.
Nilifanya
hivyo kwa imani kwamba ilikuwa bahati mbaya na angejirekebisha kama kiongozi wa kiroho, jambo ambalo ameshindwa
kulifanya kwa miaka tisa sasa tokea wakati huo.
Kila
Mtanzania mwenye akili timamu anafahamu kuwa Padri Mapunda “alikemea tabia ya kupeana
uongozi ndani ya familia moja” baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kupitisha
majina ya wanafamilia yake kugombea nafasi za kisiasa katika chama hicho.
Walioteuliwa
kugombea ujumbe wa NEC kwa wilaya za Lindi Mjini na Bagamoyo, mkoa wa Pwani na
kumwibua padri huyo kusema hayo ni mke wa Rais, Mama Salma Kikwete na mtoto
wao, Ridhiwani Kikwete.
Wote
pia hawakupata wapinzani katika kinyang’anyiro hicho na kisha wakashinda siku
za uchaguzi huo, lakini mwanafamilia mwingine ambaye ni mdogo wa Rais huyo, Mohammed
Kikwete aliyeteuliwa kugombea uenyekiti wa chama hicho wilayani Bagamoyo
alianguka.
Huo
ndio wivu mbaya kabisa alionao kiongozi huyo wa kiroho unaokwenda sambamba na
chuki, fitina za malengo ya kisiasa, majungu na uchonganishi unaolenga
kuwapandikizia hasira za uasi wananchi ili kukidhi matakwa yake mwenyewe na wapambe
wake.
Anafanya
kila anachoweza ili wafuasi wake wa kiroho wamfuate pia katika itikadi zake za
kisiasa na chuki zake kwa Rais Jakaya Kikwete, familia yake, CCM na Serikali ya
Awamu ya Nne.
Sitaki
niaminishwe kwa namna yoyote kuwa mahubiri yake hayo ni agizo la Kanisa
Katoliki kutoka popote, hivyo nitabaki naamini katika moyo wangu wote kwamba
hayo ni matakwa yake mwenyewe ya kisiasa na siyo ya kiroho na hata vinginevyo.
Ni
ajabu kwa padri kusimama katika altare kanisani na kusema uongo huku akiwa
ameshika Biblia Takatifu, lakini pia ni dhambi zaidi kuhubiri uzushi unaolenga
kuwachonganisha watu ili wafarakane kwa namna yoyote.
Harakati
za Mama Salma Kikwete, Ridhiwani Kikwete na Mohammed Kikwete kugombea nafasi
hizo za kisiasa katika CCM hazikuanzia mikononi mwa Rais Kikwete wala ndani ya
NEC isipokuwa wilayani wanakotoka.
Zilianzia
Lindi Mjini na Bagamoyo walikoomba kugombea nafasi hizo baada ya kujipima
wenyewe, kisha wakajiridhisha kuwa wanakidhi masharti ya Ibara ya 14(1) – (3)
ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 1977 Toleo la 2010 inayosema
ifuatavyo:
“Mwanachama
yeyote (wa CCM) atakuwa na haki ya kushiriki katika shughuli zote za CCM kwa
kufuata utaratibu uliowekwa, haki ya kuhudhuria na kutoa maoni yake katika
mikutano ya CCM pale ambapo anahusika, (na pia) haki ya kuomba kuchaguliwa kuwa
kiongozi wa CCM na ya kuchagua viongozi wake kwa mujibu wa katiba na taratibu…”.
Walifanya
hivyo kwa kuchukua, kujaza na kurejesha fomu na kuambatanisha vielelezo vyote walivyotakiwa
kuviwasilisha katika ngazi zote za mchakato huo mrefu ulioanzia wilayani,
mkoani hadi kwenye vikao vya kitaifa ambako uteuzi wao ulifanywa kwa kuzingatia
Katiba ya CCM na siyo kwa matakwa ya Kikwete au ya familia yao .
Wote
wanakubaliana na masharti yote ya Ibara ya 5(1) – (19), na pia wanakidhi
matakwa ya Ibara ya 7, 8(1) – (7), 12(1) – (2) na 15(1) – (9) za katiba ya
chama chao hicho na masharti yote yaliyotajwa na Ibara ya 2(1) – (2), 3(1) –
(2) na 5(1) – (2)(a) – (d) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
Mwaka 1977 Toleo la 2005 inayotumika sasa.
Kabla
ya kuteuliwa na NEC kugombea nafasi hizo, hatua ambayo pia haikuwa ya mwisho ya
kuzipata nyadhifa hizo ila hadi wawili kati yao waliposhinda katika uchaguzi
mkuu wa ngazi zinazohusika, kila mmoja alipaswa kujitetea mwenyewe kwa Wajumbe
wa Mkutano Mkuu wilayani kwake ili kuomba wamchague, hivyo ni uzushi na uongo
mkubwa kudai eti kuwa kuna tabia ya “kupeana uongozi ndani ya familia moja” katika
CCM.
Hata
Rais Kikwete naye akitaka kugombea nafasi yoyote katika chama hicho hapewi tu wadhifa
huo na familia yake iwe na mkewe, watoto wake, wadogo zake, wajomba zake,
shangazi zake, binamu zake, mama zake, baba zake wala vinginevyo.
Itabidi
atimize masharti yote ya Ibara ya 5(1) – (19), 7, 8(1) – (7), 12(1) – (2) na
15(1) – (9) za Katiba ya CCM na matakwa yote yanayotajwa na Ibara ya 2(1) –
(2), 3(1) – (2) na 5(1) – (2)(a) – (d) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Mtu
anapokurupuka na kudanganya utadhani ni mganga wa kienyeji kama alivyofanya
Padri Mapunda anakuwa moja kwa moja ni mzandiki kinywani na amesheheni wivu
mwili mzima, chuki binafsi, uchonganishi na uchochezi kwa misingi ya kisiasa.
Ndiyo
maana anadanganya pia kwamba eti viongozi wa serikali ya CCM waliua Azimio la
Arusha na kuligeuza kuwa “azimio la wala rushwa na ufisadi” huku akijua
anaongea uongo.
Kama
ambavyo lilianzishwa mwaka 1967 na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya
vyama vya Afro – Shiraz Party (ASP) cha Zanzibar na Tanganyika African National
Union (TANU) cha Tanzania Bara, wakati huo vikiwa ni vyama pekee vya siasa kila
upande kabla ya kuungana na kuwa CCM ilipofika mwaka 1977, azimio hilo pia
lilifanyiwa marekiebisho mapya ya msingi mwaka 1992 kwa njia zote halali.
Sababu
kubwa zaidi iliyosababisha kufanywa kwa marekebisho hayo ni Tanzania kuingia katika mfumo wa
vyama vingi vya siasa, jambo ambalo linaelezwa katika Ibara ya 3(1) – (2) ya
Katiba ya nchi hii.
Padri
Mapunda mwenyewe anajua kwamba Azimio la Arusha ni imani ya kisiasa ya TANU na
ASP na baadaye CCM, hivyo isingewezekana liendelee kuwepo hata baada ya nchi
kuwa ya vyama vingi kwani kila chama kinakuja na imani, itikadi na sera zake.
Ndiyo
maana mwaka 1992, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyokutana Zanzibar iliona haliwezi tena kuendelea,
badala yake likabaki kuwa ni dhana inayotajwa katika Ibara ya 3(1) ya Katiba ya
nchi inayosema kwamba “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya
kijamaa, isiyokuwa na dini na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa”.
Kana
kwamba haitoshi, padri huyohuyo na Watanzania wengine wanafahamu namna gani vyama
mbalimbali vya siasa vinavyopingana, vile ambavyo kuna vingine havitaki Tanzania
iendelee kuitwa “nchi ya kijamaa” kwa sababu hiyo ni itikadi ya kisiasa ya CCM.
Vipo
vinavyotaka neno hilo
liondolewe kwenye Katiba, hivyo endapo lingekuwepo hadi sasa ingekuwa fujo,
vurugu na kutumika kuwa kichaka cha baadhi ya watu kuitukana CCM, serikali na
viongozi wake, hivyo ni uongo mkubwa kudai limegeuzwa kuwa “azimio la wala
rushwa na ufisadi” ila ni chuki zake mwenyewe za kisiasa.
Aidha,
siyo kweli kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alifanya kazi peke yake ya
kuwaondoa wakoloni hapa nchini, badala yake ilifanywa na Watanzania wote waliokuwepo
wakati huo. Tunachoweza kusema ni kwamba yeye alikuwa ni kiongozi wao kupitia
chama cha TANU kwa Tanzania Bara, halafu Sheikh Abeid Amaan Karume aliyekuwa Rais
wa ASP akiongoza mapambano hayo huko visiwani Zanzibar .
Kuhusu
madai kuwa wakati wote wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza
haukuwepo mgomo wowote, Padri Mapunda pia aliamua kuzungumza uongo huo kwa
sababu ya chuki hizohizo, hasira za mgombea urais aliyekuwa akimuunga mkono
mwaka 2010 kushindwa vibaya, hali iliyoepusha kuundwa kwa serikali ya ubaguzi wa
kidini na hasa ukatoliki nchini.
Mwaka
1967, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
akiwemo aliyekuja kuwa Spika wa Bunge mwaka 2005, Samwel Sitta waligoma kwa
madai ya kisiasa dhidi ya Serikali ya Awamu ya Kwanza ,
kisha wakatimuliwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe hadi walipokuja kumwangukia na
kuomba radhi.
Aidha,
hakuna ubishi kwamba wakati wote wa Operesheni Vijiji vya Ujamaa mwaka 1974, maelfu
ya Watanzania walishurutishwa kuhama kwenye makazi yao
ya asili huku nyumba zao zikichomwa moto kwa mtutu wa bunduki, na pia kuna
wengine walipigwa risasi na kujeruhiwa kwa namna moja ama nyingine hasa
waliokuwa wakigomea zoezi hilo .
Ilipofika
mwaka 1982, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi
waliopelekwa wilayani Tarime, mkoa wa Mara, walitumia nguvu za ziada kuzima
uasi na kumwaga damu dhidi ya raia waliokuwa wakivunja sheria na kutotii
mamlaka ya serikali iliyokuwepo madarakani kwa kuwapiga risasi.
Akihutubia
kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM mwaka 1986, wakati huo akiwa Mwenyekiti
wa Taifa wa Chama hicho, Mwalimu Nyerere pia aliunga mkono mauaji yaliyofanywa
na askari hao wa FFU kwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero mkoani
Morogoro waliokuwa wamegoma, kufanya vurugu na kuandamana kinyume cha sheria.
“Kazi
ya bunduki ni kuua, kumbe zipo kwa ajili ipi? Kama watu hawataki kutii sheria
za nchi hata kama ni mbovu, wanapambana na
polisi hapo unadhani askari watafanya nini wakati wana silaha hizo mikononi?”
Alisema Mwalimu Nyerere alipokuwa akiitetea Serikali ya Awamu ya Pili kwa
kupambana kikamilifu na uvunjifu wa sheria kwa makusudi.
Katika
hali hiyo, ni uongo mkubwa kudai kwamba mauaji dhidi ya watu wanaofanya hivyo
yameanza wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne, na pia ni uzushi kuwa
Baba wa Taifa aliwaunga mkono wendawazimu wachache wanaovunja sheria kwa
kutotii mamlaka zilizopo madarakani.
Kama
Padri Mapunda angekuwa halitumii Kanisa Katoliki kuhutubii siasa za
uchonganishi, uchochezi na ubaguzi asingefanya ubaguzi wa kidini na chuki,
badala yake angefuata nyayo za bosi wake hata kama
kwa kuvunga, Mhashamu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye ni Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam anakofanya kazi katika Parokia ya Manzese.
Lakini
kwa sababu ana ubaguzi wa kidini na itikadi za kisiasa, Padri Mapunda amekuwa
hasemi chochote wakati viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
wanapotoa kauli za uchochezi na hatari.
Hakusema
chochote wakati Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa alipotangaza kwa
kinywa chake mwenyewe, tena hadharani kuwa Tanzania isingetawalika
aliposhindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Alisema nchi ingemwaga damu,
na kwamba Rais Kikwete kamwe asingefika hadi mwaka 2015 akiwa bado madarakani
ila angeng’olewa kwa mabavu kinyume cha sheria na katiba ya nchi hii.
Hakusema
chochote pale Mbunge wa Arumeru Mashariki mkoani Arusha, Joshua Nassari
aliposema mkutanoni kwamba Chadema ina mpango wa kufanya uhaini wa kuitenga
mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro na kuanzisha Jamhuri ya Watu wa Kaskazini.
Naamini
hakuwakemea kwa sababu ya itikadi za kisiasa, upendeleo na ubaguzi wa kidini kwa
sababu ni wakristo wenzake huku Dk. Slaa akiwa padri wa zamani wa Kanisa
Katoliki, halafu Nassari ni mtoto wa Mchungaji Samwel Nassari wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mlima Meru.
Hakukemea
mauaji yaliyofanywa na polisi kwenye Msikiti wa Mwembechai jijini Dar es Salaam
mwaka 1997, na pia hakusema chochote baada ya mauaji ya Pemba
mwaka 2001 kwa vile Rais aliyekuwepo madarakani wakati huo, Benjamin Mkapa ni muumini
wa Kanisa Katoliki.
Hafanyi
kama Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea
watu wote wanaovunja sheria, kuhatarisha amani au kutoa kauli za uchochezi bila
ya kujali imani zao kiroho na kukemea matendo yote maovu.
Amekuwa
akiwa akifanya hivyo huku akiwataka watu wote kuheshimu sheria za nchi, kutii
mamlaka au serikali inayokuwepo madarakani kwa vile zote “zinawekwa na Mungu” kama inavyosema Biblia Takatifu.
Kabla
sijafikia mwisho, sasa ninaomba nionyeshe kuwa kauli ya Padri Mapunda ya
kukemea kile alichodai ni “tabia ya kupeana uongozi ndani ya familia moja” siyo
lolote wala chochote ila ni uzandiki, fitina, uchochezi na harakati zake za
kisiasa dhidi ya CCM.
Wakati
wa kutafuta wabunge hao mwaka 2010, Kamati Kuu ya Chadema iliyafuta matokeo
halali ya washindi waliopigiwa kura na akina mama wenzao katika Baraza la
Wanawake la Chama hicho (BAWACHA), uchaguzi ambao ulifanyika kikatiba katika
Ukumbi wa PTA uliopo kwenye Uwanja wa Sabasaba, Mtoni jijini Dar es Salaam .
Katika
uchaguzi huo uliosimamiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ambaye pia ni Mshauri wa Kisiasa
wa Chadema na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Mkumbo Kitilya, washindi
wengi waling’olewa kwa sababu tu walitoka kwenye kambi inayomuunga mkono Mbunge
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Waling’olewa
kwa sababu hawakutoka kambi ya Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu,
Dk. Wilborad Slaa na viongozi wengine wa kitaifa. Hapo ndipo uchaguzi huo
ulipofutiliwa mbali na badala yake, wabunge hao wakateuliwa ofisini kwa kuangalia
familia zao au mahusiano mengine kati yao
na viongozi waandamizi wa chama hicho.
Baadhi
ya wabunge hao ni Rose Kamili ambaye ni mke wa Dk. Slaa, Christina Lissu (dada
yake na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu) na
Raya Ibrahim Khamis, mtoto wa dada yake na Makamu Mwenyekiti wa Chadema
(Zanzibar), Saidi Issa Mzee.
Wengine
ni Mhonga Saidi (binamu yake Zitto), Anna Komu (shemeji yake Mkurugenzi wa
Fedha na Utawala, Anthony Komu), Lucy Owenya (binti wa Mwenyekiti wa Chadema wa
Mkoa wa Kilimanjaro na Mjumbe wa Kamati Kuu, Philemon Ndesamuro) na Grace
Kiwelu ambaye ni mke wa mtoto wa Ndesamburo na kadhalika.
Huu
ndio uongo, uzushi, umbeya na uzandiki unaofanywa na Padri Baptiste Mapunda
dhidi ya CCM na serikali yake, ule ambao unakwenda sambamba na mapenzi yake makubwa
ya kisiasa kwa Chadema katika upande wa pili!
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi,
Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0659
220 220 na 0762 633 244