Tuuchukieni uongo, uzushi na unafiki mkubwa wa Chadema Na Charles Charles MBUNGE wa Rombo mkoani Kilimanjaro kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Selasini aliusifia utendaji maridadi wa kazi unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete. Selasini alitoa kauli hiyo wakati wa sherehe za uzinduzi wa Barabara ya Mkuu – Tarakea wilayani humo, siku chache zilizopita na kuwashambulia hadharani wanasiasa ambao alisema wamezoea kudandia migongoni mwa wenzao. “Nina kila sababu ya kukushukuru na kukupongeza”, alisema mbunge huyo na kuongeza kuwa kama angekuwa na uwezo angeipa barabara hiyo “jina la Jakaya Kikwete” kwa vile ndiye ametoa fedha zilizotumika katika ujenzi huo, ule uliotimiza ndoto ya miaka mingi ya wananchi wa Rombo. “Barabara hii imekuwa kwenye makabrasha tangu enzi za ukoloni, lakini Rais Kikwete ametimiza ndoto ya Warombo ya kuungana tena na wenzao kwa shughuli za kibiashara”, alibainisha. Kesho yake, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe naye alimsifu hadharani Rais Kikwete alipokwenda na kuzindua Barabara ya Kwa Sadala – Masama iliyopo katika jimbo hilo. Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa kazi kubwa na yenye mafanikio ya kujenga miundombinu ya barabara nchini na kumuunga mkono Rais Kikwete binafsi na kuongeza: “Huyu ndiye kiongozi wetu, ndiye mkuu wetu, mkuu wa nchi yetu na haijapata kutokea katika historia ya Tanzania. Mmefanya kazi kubwa sana katika kuiunganisha nchi yetu kwa mtandao mkubwa wa barabara. Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais”. Wakati viongozi hao waandamizi wa Chadema wakisema hivyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Taifa wa Chama hicho, John Mnyika alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akitaka aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), William Mhando ashtakiwe mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali ya umma. Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo jijini Dar es Salaam, amekuja na msimamo huo mpya wa Chadema miezi miwili tu baada ya Naibu Katibu Mkuu wake (Tanzania Bara), Zitto Kabwe aseme kuwa hatua zote zilizochukuliwa na serikali dhidi Mhando zilifanywa kinyume cha taratibu. Aidha, Zitto yuleyule ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alikuwa akimtetea kwa nguvu zake zote kiongozi huyo wa zamani wa TANESCO akidai alikuwa amegeuzwa na serikali kuwa “mbuzi wa kafara”. Hao ndio viongozi wa Chadema ambao ukimwondoa Selasini, watatu waliobaki wote wanapozungumza chochote ndio msimamo wa chama chao kwa vile ni Mwenyekiti wa Taifa, Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Taifa wa Habari na Uenezi. Nimeshangazwa na kauli zao mpya kutokana na ukweli kuwa wote katika ujumla wao ni mitambo inayotegemewa kuzalishia uongo, fitina, uzushi, uchochezi na umbeya unaolenga kuwapandikizia hasira na chuki Watanzania ili waichukie serikali inayotawala hivi sasa. Wote wamejitokeza kuwa mabingwa wa kuhamasisha uasi dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wake, lakini kazi hiyo yote inafanywa kwa makusudi na malengo ya kutaka nchi isitawalike katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015. Mbowe na Selasini waliomsifu Rais Kikwete na serikali yake, wakampamba kwa vinywa vyao majukwaani, wakakiri ubora na utendaji wake maridhawa ndio walewale ambao walifanya uchochezi mkubwa na kuongoza maandamano ya vurugu, ghasia na uhalifu wa aina zote katika jiji la Arusha hapo Januari 5, mwaka jana. Walifanya hivyo wakishirikiana na viongozi wengine wa Chadema kama vile Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa; Wajumbe wa Kamati Kuu akina Philemon Ndesamburo, Godbless Lema, Grace Kiwelu, Peter Msigwa na kundi zima la wabunge walionao. Kutoka Arusha waliendeleza vurugu zao hizo katika mikoa mingine ikiwemo ya Mwanza, Kagera, Shinyanga, Iringa, Njombe na kadhalika ambako pia walikwenda wakitangaza kila aina ya uzushi, unafiki pamoja na uzandiki wote unaoweza kuwatoka midomoni mwao. Walikuwa wakitangaza kuwa serikali ya CCM imeshindwa kuwaletea maendeleo yoyote wananchi katika kipindi chote cha miaka 50 ya Uhuru uliopatikana Desemba 9, 1961, na kutaka mwaka 2015 wapewe madaraka hayo wao ili waiendeleze kwa kasi. Walisema Tanzania haina miundombinu ya barabara hasa za lami au changarawe, maji safi na salama ya kunywa huku pia ikizidi kurudi nyuma katika maendeleo mengine yakiwemo ya elimu. Kibaya zaidi walifikia mpaka kudai kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ikiongozwa na Rais Kikwete yuleyule ndiyo “ziro zaidi”. Waliwataka Watanzania bila ya kujali itikadi zao za kisiasa waitikie wito wao wa kutaka nchi isitawalike katika kipindi chake hiki cha pili, na pia wakamwambia yeye mwenyewe hatafika mwaka 2015. Wamekuwa wakipandikiza kila aina ya uasi, fitina, uzushi, hasira na chuki kwa rais huyo mwenyewe, CCM na serikali yake wakitaka wananchi wawaunge mkono na kumwondoa madarakani ikibidi hata kinyume cha katiba ya nchi! Wanatumia njia zote wanazodhani zinafaa, moja kati yake ni kile kinachoitwa ‘Operesheni Sangara’ iliyokuja kuongezewa jina kuwa ni ‘Vuguvugu la Mabadiliko’ au ‘Movement for Change (M4)’, kazi ambayo siku zote imekuwa ikitumika kutengenezea uongo na fitina za kijinga. Pamoja na kusafiri kwa barabara kutoka Dar es Salaam hadi mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Lindi, Mtwara, Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara na kadhalika kwa kupita kwenye lami huku wakisinzia sehemu kubwa ya safari, viongozi wa Chadema wanapofika waendako husahau hayo yote utadhani kuku wa kisasa. Wanaanza kuzitukana barabara walizopita wakidai kuwa ni mbovu huku nyingi kati yake zimejaa mashimo na mabonde, zile ambazo utakuta wanadai wanalazimika kusafiri kutoka mwanzo hadi mwisho wakiwa wamefunga vioo vyote vya magari yao ili kukwepa vumbi. Hawasemi ukweli kwamba wanafunga madirisha yote ili kukwepa upepo kwa sababu zina lami na hivyo magari yao yanakwenda kasi zaidi. Hawataki kusema kwamba siku zote wanaamshwa wakiwa tayari wameshafika waendako na kubaki wanashangaa wamefikaje kwa haraka namna hiyo! Usingizi mzito wanaolala wakati wote wanapokuwa safarini, huwafanya wasione kwa uhakika namna gani barabara za nchi hii zilivyojengwa katika kiwango cha lami, hali inayosababisha waseme uongo wanapopanda majukwaani. Wanazungumzia hadithi za miaka mingi iliyopita walipokuwa wakisafiri kuelekea shuleni kama Mbowe aliyekuwa akitokea kwao Hai, Kilimanjaro au Dar es Salaam kwenda Shule ya Sekondari ya Kahororo, Bukoba. Anadhani hali bado iko vilevile kwa sababu akisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Lindi, Mtwara, Iringa, Mbeya, au Singida anakuwa amelala kwa muda mwingi kwenye gari na kushindwa kuyaona maendeleo makubwa ya miundombinu ya barabara yaliyofanywa na serikali ya CCM. Ndiyo maana anapofika huko anaanza kuwadanganya wakulima na wafugaji ambao kwao wanapokwenda mbali sana ni kutoka vijijini mwao hadi makao makuu ya kata zao, tarafa zao, wilaya zao au mikoa yao ambapo kwa kawaida huwa siyo zaidi ya kilomita angalau 10 tu. Mwanasiasa mwandamizi kama Mbowe kwa mfano akitangaza kwamba ametokea Dar es Salaam hadi Iringa na kujionea ubovu wa barabara alimopita, akadai imejaa mashimo kila mahali, mabonde na majani utadhani ina mashamba hakika mwananchi anayeishi siku zote maeneo ya Kihesa, Ruaha, Kitwiru, Mtwivila, Mwangata, Mkwawa au Nduli inakuwa kazi rahisi mno kuuamini uongo huo na kwenda kuutangaza kwa majirani zake. Hivyo ndivyo wanavyofanya viongozi waandamizi wa Chadema akina Freeman Mbowe, Dk. Wilbroad Slaa, Zitto Kabwe, John Mnyika, Peter Msigwa, Godbless Lema, Vencent Nyerere, Grace Kiwelu, Joseph Mbilinyi au ‘Mr. Sugu’ na kadhalika. Ndiyo maana pia miezi mitano tu iliyopita, Mbowe aliwaambia wananchi wa Lindi kuwa anakerwa na kushangazwa na miundombinu mibovu ya barabara nchini. Alisema hali hiyo haiwezi kurekebishwa hata iweje kama CCM itaendelea kutawala, hivyo akatangaza kwamba atazunguka kila kona akiwaomba wananchi wakiunge mkono chama chake ili mwaka 2015 kitawale na kusema anaamini wataelewa, kisha akaahidi kujiuzulu endapo watashindwa tena katika uchaguzi huo mkuu. Alisema kuwa atafanya hivyo kwa vile Watanzania watakuwa “wamemwambia kwamba wamezoea kuishi kwa taabu” bila ya barabara ambazo zimejengwa kwa lami. Atakuwa ameelewa kwamba “hawataki nchi yao ipate maendeleo” isipokuwa vinginevyo. Katika hali hiyo, Mbowe ambaye kuna wengine wanamwelezea kuwa ni rasta wa zamani ndipo akaahidi kujiuzulu nyadhifa zake zote za kisiasa, nafasi ambayo itatoa fursa kwake ya kurudi upya kwenye shughuli za kasno la Billicanas Night Club kusimamia tena disko lake kama mwanzo. Lakini kwa vile uongo siku zote haudumu kwa muda mrefu, yeye na Selasini hatimaye wametubu kuwa yote wanayokwenda wakiyasema nchini ni unafiki mkubwa walionao vinywani, uzushi na uzandiki uliojaa kila aina ya ushetani midomoni mwao. “Nina kila sababu ya kukushukuru na kukupongeza Mheshimiwa Rais”, alisema Selasini na kuongeza kwamba endapo angekuwa na uwezo angeipa Barabara ya Mkuu – Tarakea “jina la Jakaya Kikwete” ili kuutambua, kuuthamini, kuuhesimu na kuuenzi uongozi wa serikali yake. Mbunge huyo alisema kuwa angefanya hivyo kutokana na ukweli kwamba barabara hiyo ilishindakana tangu utawala wa kikoloni, lakini imekuja kujengwa na Serikali ya Awamu ya Nne, tena baada ya Rais Kikwete kuahidi hivyo kiasi cha miaka miwili tu. Aidha, Mbowe naye alimsifu pia Rais Kikwete kwa kicheko chote alipozindua Barabara inayotoka Kwa Sadala kwenda Masama, akaipongeza Serikali akisema kwamba imefanya kazi kubwa na ya mafanikio kwa kujenga miundombinu ya barabara nchi nzima. “Huyu ndiye kiongozi wetu, ndiye mkuu wetu, mkuu wa nchi yetu na haijapata kutokea katika historia ya Tanzania. Mmefanya kazi kubwa sana katika kuiunganisha nchi yetu kwa mtandao mkubwa wa barabara. Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais”, alibainisha mbunge huyo wa Hai, Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema. Kama nilivyoainisha mwanzo, huo ndio ujuzi na utalaamu wa unafiki mkubwa walionao viongozi wa Chadema. Wamejaliwa vipaji vya hali ya juu wanavyoweza kuvitumia wakati wowote, mahali popote na kwa namna yoyote ile kuwapandikizia hasira na chuki wananchi ili kukidhi matakwa yao, lakini wanafanya hivyo wanapokwenda nje ya kwao. Hawataki wanapokuwa majimboni kwao waonekane waongo, wanafiki wala wazushi kwa kuhofia kukosa kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hivyo wanalazimika kusema ukweli kwamba serikali ya CCM imefanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi, moja kati yake ni kujenga mtandao mkubwa wa barabara nchini kote kama alivyobainisha Mbowe. Wanakiri uongozi bora, umakini na uchapakazi mkubwa alionao Rais Kikwete na serikali yake, ile ambayo inajitahidi kutekeleza haraka ahadi inazotoa na kutamani apewe heshima zote anazostahili kama kumbukumbu ya kizazi kilichopo na vijavyo. Nani alitarajia kuwa Mbowe au Selasini wangetamka maneno hayo hadharani, tena ikiwa ni siku chache tu baada ya kutoka kuwapandikizia hasira, uchochezi na chuki wananchi dhidi ya CCM na serikali yake, kazi waliyokuwa wakiifanya usiku na mchana wakati wa kampeni za chaguzi ndogo za udiwani zilizofanyika nchini kote hivi karibuni? Mbali na hayo, vilevile niligusia unafiki mkubwa wa Chadema kuhusiana na suala zima la mgogoro wa kikazi uliokuwa ukimkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, William Mhando ambaye hatimaye aliondolewa katika wadhifa huo, Jumatatu ya wiki iliyopita. Wakati aliposimamishwa na serikali ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, viongozi wa Chadema wakiwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wao, Zitto Kabwe walijitosa kumtetea sana wakidai kwamba alikuwa “ametolewa sadaka” au “mbuzi wa kafara”. Walifanya kila wanavyoweza ili kuwadanganya Watanzania eti kwamba serikali ya CCM inakumbatia uozo katika shirika hilo la umma, hivyo kwa vile Mhando alitaka kupambana nao kwa juhudi na maarifa yake yote akaundiwa tuhuma za kutunga ili hatimaye afukuzwe kazi. Walijaribu kufanya hivyo ili kuendeleza mfumo wao wa siku zote wa kufanya siasa za kitapeli, uzushi, uchochezi na ubaguzi unaolenga kuwagawa Watanzania katika misingi ya ukabila, ukanda na kutaka wakati wote waipinge serikali hata kama inatimiza wajibu wake kwa njia zote halali. Chadema iliyokuwa mstari wa mbele kumtetea kwa upotoshaji sana wakati huo ndiyo ileile iliyokuja kuwa ya kwanza kutaka ashtakiwe mahakamani. Imefanya hivyo kwa kutafuta umaarufu ili baadaye endapo atafunguliwa kesi ije iwadanganye watu kuwa imeilazimisha yenyewe serikali. Nasema huu ni unafiki kwa sababu haiwezekani mwanzo chama hicho kisimame kidete na kuwatangazia uongo wa makusudi wananchi, kikamtetea sana kuwa ametolewa sadaka au mbuzi wa kafara ili kuficha uozo wa serikali, lakini ilipokuja kuthibitika kuwa ana tuhuma za jinai kiwe cha kwanza kumnyoshea kidole. Chama cha siasa kinachokuwa na viongozi wanafiki wakubwa kiasi hicho, kisha siku zote kikawataka wapiga kura wakiamini ili wakiweke madarakani ni hatari. Kama vinavyosema vitabu vitukufu, mtu anaposhuhudia uovu wa aina yoyote ukitendeka mbele yake hana budi aukemee kwa ulimi wake mwenyewe. Kama hawezi kuukemea anapaswa auzuie kwa mikono yake mwenyewe, lakini kama hawezi pia kuuzuia kwa njia hiyo basi angalau aukasirikie tu. Hivyo ndivyo Watanzania wanavyopaswa kufanya dhidi ya viongozi wa Chadema. Inabidi angalau wauchukie uongo, uzushi na unafiki wao wote! Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244