• CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM CHAMA MAKINI KINACHOFANYA MAAMUZI KWA VIKAO RASMI
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA

Watajiliwaza magazetini siku zote, lakini Chadema ni kama nyuki wa mashineni tu

Na Charles Charles AKIANDIKA makala yake kwenye gazeti moja la kila Jumatano wiki iliyopita, Mshauri Mkuu wa Kisiasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Kitila Mkumbo alidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimenza kunasinyaa! Mkumbo ambaye amekuwa akikwepa kujitambulisha kwa cheo chake hicho, badala yake akijibainisha tu kuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lengo likiwa ni kutaka wananchi waone chama hicho kinaungwa mkono hadi na wasomi wa ngazi yake, alikuwa akizungumzia matokeo ya chaguzi ndogo za udiwani zilizofanyika wiki mbili zilizopita. Alisema wakati CCM ilishinda kata 22 kati ya 29 zilizokuwa zikigombewa, Chadema ilipata tano ambazo kati yake; mbili ilizitetea “zake” huku tatu ikiinyang’anya CCM. “Kimahesabu ushindi wa viti vitatu vitatu ni mdogo mno ukilinganisha na mvuto ambao Chadema hivi sasa inao. Vilevile, kupoteza viti vinne siyo jambo la kutisha kwa chama kilichochokwa kama CCM. Hivyo hitimisho ambalo tunalipata ni kwamba Chadema inakua na CCM inasinyaa”, anaandika kiongozi huyo tegemeo propaganda kwa chama chake hicho. Siku ileile, mwandishi wa habari kwenye gazeti moja la kila siku nchini aliandika makala yake akisema “CCM inabidi imeguke ili iweze kushinda mwaka 2015”, vinginevyo itazama. Anasema uchaguzi mkuu wa ndani ya CCM unaohitimishwa Jumanne ijayo, “umetia petroli kwenye moto” kwa kuimarisha makundi ambayo yanajipanga kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo. Akiwadanganya zaidi Watanzania anasema moja ya makundi hayo limedhihirsha kuwa na nguvu kimkakati, mipango na mbinu baada ya wagombea wake wengi kushinda hadi ndani ya jumuia za CCM ambazo ni Umoja wa Vijana (UVCCM), Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Umoja wa Wazazi. Katika hali hiyo, mwandishi huyo anasema kundi hilo sasa linatakiwa liwatimue mahasimu wake kutoka chama hicho kabla ya mwaka 2015. “Wakipuuza (ushauri huu) basi wasubiri kuzama wote kwa kuwa wamo ndani ya boti inayotobolewa na wasafiri wenyewe”, anasema na kuhitimisha: “Kwa uhai na maslahi ya CCM na pengine ya taifa (zima), ni lazima chama hicho kimeguke vipande viwili na kujijenga kabla ya uchaguzi (mkuu wa mwaka) 2015”. Hivyo ndivyo Dk. Mkumbo na mwandishi huyo wa habari anayeishi Arusha wanavyosema katika makala zao hizo, zote zikiandikwa Jumatano wiki hii, lakini katika vyombo viwili tofauti. Kwanza kabisa nasema ni upuuzi kukubali ushauri wa kipuuzi maana unaweza kuwa mpuuzi na mjinga wa kufikiri, na pia ni wendawazimu mkubwa kichwani kwa mtu kuaminishwa na uongo unaochongwa kama kinyago. Kama ameingia kwa hiari katika siasa, Dk. Mkumbo hapaswi kuitetea Chadema yake kwa nguvu zake zote huku akijitambulisha kuwa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu, nafasi anayolenga kuitumia ili kuwazubaisha wananchi akianzia wanafunzi anaokuwa nao darasani. Ni vizuri akiwa anajitambulisha wazi kuwa ni Mshauri Mkuu wa Kisiasa wa Chadema ili wasomaji wake wafahamu kwamba anafanya kazi aliyotumwa. Anapaswa apambane waziwazi na si kuingia ulingoni huku akilikwepa koti la Chadema, badala yake akiandika makala za tafiti za kisomi hapo ana haki ya kujitambulisha kuwa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu chochote duniani! Kama Mshauri Mkuu wa Kisiasa ya Chadema, Dk. Mkumbo ndiye alisimamia uchaguzi wa kutafuta Wabunge wa Viti Maalum wa chama hicho uliofanyika kwenye Ukumbi wa PTA, ule ambao umo ndani ya Uwanja wa Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara wa Mwalimu Julius Nyerere, Sabasaba jijini Dar es Salaam mwaka 2010. Ni yeye aliyeandika na kisha kupeleka mapendekezo ya kutaka uchaguzi ule ufutwe, ripoti aliyowakabidhi viongozi waandamizi wa Chadema hususan Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa na kutaka wabunge hao wateuliwe mezani na siyo kuchaguana wenyewe. Alipaswa akishauri chama hicho kuwa zoezi hilo lirudiwe kwa wanawake hao kuchaguana wenyewe ili haki itendeke, lakini inawezekana hakufanya hivyo kwa vile naye alikuwa na maslahi yake binafsi au alionao watu wake wameshindwa. Baadhi ya kina mama walijitoa Chadema ili kupinga kufutwa kwa uchaguzi huo, ule ambao ulipofutwa na kisha wabunge hao wakateuliwa na wanaume, wengi kati yao walipachikwa nyuma katika orodha iliyopelekwa katika Tume ya Uchaguzi ya Taifa na kuukosa ubunge huo. Inawezekana Dk. Mkumbo naye alishiriki faulo hiyo na akina baba wenzake ili wanawake waliokuwa wakiwataka kwa maslahi yao ndio wawe wabunge, ‘bundi’ ambaye ataendelea ‘kulia’ kichwani kwake hadi mwaka 2015 au hata kwa miaka mingi zaidi. Baadhi ya wanachama, viongozi, kina mama na wafuasi wa Chadema wanaamini hadi leo kuwa uchaguzi ule ulifutwa kwa sababu idadi kubwa ya washindi walitoka katika kambi inayomuunga mkono Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe. Ulifutwa kwa vile akina mama takribani wote ambao ni watiifu kwa Mbowe na Dk. Slaa walitupiliwa mbali. Badala ya kuutolea ufafanuzi uhaini wake huo, Dk. Mkumbo amekuwa bingwa wa kuandika uzushi dhidi ya CCM na serikali yake, kazi anayolenga kuwaaminisha umbeya wapiga kura ili kusaka ushindi kwa ajili ya chama chake katika uchaguzi mkuu ujao. Anatumia usomi wake huo kwa maslahi yake binafsi, Chadema yake na harakati zake za kutaka kupata umaarufu ili akagombee ubunge katika jimbo la Iramba Magharibi mkoani Singida mwaka 2015. Ndiyo maana inadaiwa kuwa alishiriki kumtukana mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Mwigulu Nchemba (CCM) katika moja ya mikutano yao huko mwaka huu, ule ambao uliibua vurugu na kifo cha mmoja kati ya viongozi wa UVCCM wa Kata ya Ndago. Kama angekuwa muungwana, Dk. Mkumbo angewaambia ukweli wananchi kuwa ushindi wa kata tano wa Chadema yake wiki mbili zilizopita, ulitokana kwa kiasi kikubwa na CCM kutofanya kikamilifu kampeni kwa sababu ilikuwa inaendelea na uchaguzi wake wa ndani unaohitimishwa rasmi Jumanne ijayo. Alipaswa aseme kwamba ingawa chaguzi hizo zilifanyika wakati tayari katika ngazi hiyo ya kata CCM ilishapata viongozi, lakini zilikuja siku chache tu tangu walipochaguliwa, hivyo wengi wao walikuwa hawajakabidhiwa hata ofisi ili waanze kazi ikiwemo hiyo ya kuongoza chaguzi hizo za dola. Alitakiwa awaambie ukweli kwamba ushindi huo kwa CCM ulikuja huku Mbowe, Dk. Slaa, Wakurugenzi wa Taifa wa Idara zote za Makao Makuu ya Chadema ukimwondoa Anthony Komu, wabunge wake wote na kadhalika, walihamia kwenye kata zote wakifanya kampeni za kutafuta ushindi kwa muda wote. Walikuwa wamejichimbia huko kote wakienda kila kijiji na kitongoji usiku na mchana huku wakiimba kila aina ya uzushi, uongo, uchochezi na kupandikiza chuki zote dhidi ya CCM na serikali yake huku Mbowe na Dk. Slaa wakiongoza kazi hiyo yote. Ilibidi akiri kuwa kampeni hizo pia zilifanyika huku viongozi hao wote wakitokea moja kwa moja kwenye mizunguko mingine isiyoisha, ile inayoitwa ‘Operesheni Sangara, Vuguvugu la Mabadiliko’ au ‘Movement for Change’ ambayo ni maarufu zaidi kwa kifupi cha M4C. Alipaswa aeleze kuwa licha ya juhudi hizo zote zinazokwenda sambamba na kufanya vurugu, kuwakashfu viongozi wa CCM na serikali yake, kuwapandikiza hasira na chuki wananchi na kufanya uchochezi kwa kadri wawezavyo, chaguzi hizo ndogo zilipokuja kufanyika chama chake kikaambulia kata tano tu! Je, kama CCM nayo ingefanya kampeni hizo kikamilifu hapo Dk. Mkumbo anadhani hali ingekuwaje? Ni kweli kwamba angekuja na uongo huo kuwa chama hicho “kimechokwa” na wananchi au angeibua visingizio gani? Mbali na kiongozi huyo wa Chadema, mwandishi aliyedai kuwa CCM inabidi imegeuke kwanza ili ishinde uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 naye ni kama zuzu la kisiasa. Mtu asiyekuwa na matatizo kichwani mwake hawezi kupokea ushauri huo wa kijinga, hivyo endapo anatumiwa hata kama yeye hafahamu inabidi sasa awe anachambua kwanza akilini, kisha anatoa misimamo yake mwenyewe na kuacha utegemezi kwa Chadema. Ni ujinga mkubwa kufikiri kwamba iko siku ambayo utafanyika uchaguzi wowote ambao hauna makundi. Ni upeo mfupi kufikiri kuwa makundi yanayozuka katika kipindi hicho ni mpasuko unaoweza kukiathiri chama cha siasa au chochote, vinginevyo ni mtindio wa akili kudhani eti zoezi hilo popote duniani linaweza kufanyika bila ya mivutano. Tafsiri rahisi ya neno “uchaguzi” ni ushindani wa kuwania kitu kimoja, hivyo endapo wote mnakubaliana kila kitu kwa asilimia 100 sifahamu eti kwa nini mnafanya tena uchaguzi! Inakuwaje msikae kikao hata cha nusu saa tu, mkatangaziana kuwa fulani atashika nafasi hii ya uongozi, huyu atasimamia eneo lile na kadhalika, kisha mkaondoka zenu? Kwa nini Chadema iligawanyika makundi mawili mwaka 2009 wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani, likazuka kundi kubwa la Zitto na dogo la Mbowe na viongozi wenzake akiwemo Dk. Slaa, lakini mwandishi huyo hakuishauri kuwa imeguke ili ishinde uchaguzi mkuu wa mwaka 2010? Mbona Watanzania wenyewe kama taifa moja waligawanyika makundi makubwa yaliyoitwa CCM, Chadema, CUF, TLP, UDP, NCCR – Mageuzi na vyama vingine wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, lakini ulipopita wote wakabaki na utanzania wao hadi sasa? Nawaomba wana CCM nchini kote wasibabaishwe na kikundi kinachoishi kwa kujiliwaza magazetini siku zote, kile ambacho kinatumia nguvu nyingi kuonyesha kwamba Chadema inatisha wakati kumbe ni kama nyuki wa mashineni tu. Wanaweza wakaning’inia kwa wingi darini na kutengeneza masega ya asali, wakarukaruka na kupiga kelele nyingi, lakini hata siku moja hawana madhara yoyote! Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

This entry was posted in

Leave a Reply