• CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM CHAMA MAKINI KINACHOFANYA MAAMUZI KWA VIKAO RASMI
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA

Wabunge hawa wenye kazi ya kuchochea uasi na kususia vikao vya bunge ni laana

 







Na Charles Charles

IJUMAA iliyopita, wabunge wote wa kambi ya upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliokuwa kwenye kikao cha nne cha mkutano unaoendelea sasa mjini Dodoma, walitoka nje ya ukumbi na kwenda kuongea na waandishi wa habari kwa dakika 38.

“Tumewaita kuzungumzia sababu za kutoka nje na hatua za kuchukua. Kama mlivyosikia, (James) Mbatia (ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa anayetoka NCCR – Mageuzi) alisema hakuna mitaala na (wala) haijawahi kuwepo tangu mwaka 1961 na kama ipo atajiuzulu”, alisema aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho na Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Alidai kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema uongo bungeni kwamba wizara yake ina mitaala ya masomo kwa shule za sekondari na msingi, lakini akashindwa kuitoa.

“…Tutapeleka taarifa ya kikao chetu katika Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kumtaka Waziri Kawambwa ajiuzulu kwa kulidanganya bunge, ikishindikana tutaipeleka tena katika mamlaka zilizomteua”, alibainisha.

Aliongeza kuwa endapo mamlaka hiyo pia haitamwajibisha, wabunge hao watapiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili kuilazimisha serikali nzima ijiuzulu, hatua itakayomfanya Rais Jakaya Kikwete ateue baraza jipya la mawaziri kama ilivyokuwa Februari 6, 2008 wakati aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa alipoamua kujiuzulu kwa kuwajibika kisiasa.

Mbali na kufanya hivyo dhidi ya Pinda, wabunge hao waliwaambia waandishi wa habari kwamba wataandaa hoja nyingine ya kuwang’oa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu Spika, Job Ndugai kwa tuhuma za kukandamiza hoja zao.

“Tulitaka kujadili hoja ya gesi ya Mtwara, lakini Spika akaizima, akasema itaundwa tume, baadaye tume hakuna baada ya Waziri Mkuu kwenda (huko). Tangu Mbatia awasilishe pia hoja yake inaonyesha waziwazi (kwamba nayo) wanataka kuizima”, alisema Tundu Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani katika bunge hilo la 10.

Nasema siyo lazima mtu awe mpaka mwanasheria, daktari wa falsafa au profesa wa fani yoyote ndipo aweze kuuona ujinga unaofanywa na kambi hiyo ya upinzani isipokuwa hata akisoma kwa kawaida.

Haiwezekani kwamba serikali bado haina mitaala ya elimu nchini tangu nchi yetu ipate Uhuru wake mwaka 1961 hadi leo, madai ambayo ni uongo uliovuka mpaka na kuwa ni uzandiki unaotia ukakasi hata kuuzungumza mdomoni.

Ingawa ni kweli kuwa mimi siyo mwalimu na kamwe sikusudii kufanya kazi hiyo hata siku moja hapo baadaye, lakini najua mitaala ya masomo kwa shule za msingi na sekondari hapa nchini ipo, hivyo anayesema vinginevyo ingekuwa bora kama angetuambia kwamba anayodai yeye imechelewa kuanza na kueleza imechapishwa lini ili umma ufahamu. 

Nilipokuwa nasoma mwaka ule wa mwisho wa elimu yangu ya msingi nilichukuliwa na mjomba wangu aliyekuwa mwalimu mkuu shuleni kwetu, hivyo nilikuwa naziona nakala za mitaala hiyo ambayo haikuwa ya mwaka 1960, 1959 au 1958 ya kabla ya Uhuru kwa sababu hata marehemu mama yangu mzazi alikuwa bado ni mtoto wa miaka 11 tu wakati Tanzania Bara inajitawala hapo Desemba 9, 1961.

Nilikuwa naishi palepale shuleni na mjomba wangu huyo na baadhi ya walimu, hivyo nilikuwa pia naona wakiandaa masomo ya kwenda kutufundisha madarasani siyo kwa matakwa yao wenyewe, bali walitumia mitaala hiyo ya elimu inayotungwa serikalini. 

Mbatia aliyeshindwa kukijenga chama chake ambacho yeye ndiye Mwenyekiti wa Taifa anadhani atakijenga kwa kuwasilisha hoja hizo za uongo na uzushi bungeni. 

Anadhani kwa kufanya hivyo kitafufuka tena kama ilivyokuwa Februari 28, 1995, siku ambayo aliyewahi kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Augustine Lyatonga Mrema alipohamia huko akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na uchu wake wa kutaka kugombea urais.

Anadhani kitafufuka na kuwa na nguvu kiliyodumu nayo kuanzia hapo hadi mchana wa Jumapili Aprili 25, 1999, siku ambayo Mrema alitangaza ghafla tena kuachana na chama hicho na kuhamia Tanzania Labour Party (TLP) na kusambaratika nchi nzima siku ileile.

Endapo anatumia hoja hiyo akidhani itamjenga kisiasa au chama chake basi aelewe kuwa amedanganywa kama mtoto anayesoma shule ya chekechea. Ni vizuri akimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kumteua kushika nafasi hiyo, ile ambayo alijitosa kuigombea mwaka 2010 katika jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam na kushindwa vibaya.

Anapaswa ajue kwamba hakuteuliwe ili akafanye utapeli wa kisiasa bungeni, ule ambao ni pamoja na kudai Tanzania haijawahi kuwa na mitaala katika shule za msingi na sekondari tangu ipate Uhuru wake mwaka 1961!

Aliteuliwe kuwa mbunge ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 66(e) na 67(a) na (c) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Toleo la 2005 inayotumika sasa. 

Hakuteuliwa kwenda kutumia nafasi hiyo ili kusema uongo, uzushi, umbeya wala kufanya uchochezi wowote au uchonganishi kati ya Watanzania na serikali ya nchi yao. 

Haiwezekani kwamba eti Waziri wa Elimu awe anazunguka na mzigo wa nakala za mitaala ya shule kila anakokwenda iwe bungeni, ndani ya vikao vya kiserikali ama pale anaposafiri kikazi nje ya nchi ili kama atatakiwa kuzungumzia suala hilo anazionyesha papo kwa papo.

Kama alivyosema hata Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, serikali katika kikao kilichopita iliahidi kuwasilisha mitaala hiyo katika kikao hiki cha sasa na kuhoji: “Sasa wasiwasi wa mbunge (Mbatia) ni nini? Tutaileta hata siku ya mwisho ya bunge”.

Tayari serikali imewasilishwa bungeni jana, Jumatano ambapo kila mbunge anatakiwa kupata nakala yake mwenyewe.

Sipendi kuamini kuwa Mbatia, Tundu Lissu, Mrema na wabunge wengine wote waliotoka nje ya bunge, Ijumaa iliyopita ni kama watoto wa chekechea katika kuchanganua mambo. Sitaki kabisa niamini kwamba akili yao bado nyembamba wakati wote wana umri wa zaidi ya miaka 18. 

Mchukulie Mrema kwa mfano ambaye kama asingekimbilia bungeni angekuwa tayari ni mtumishi mstaafu wa umma kwa vile miaka yake duniani iko kwenye 70. Leo naye eti anaunga mkono upuuzi wa vijana kama Mbatia aliyezaliwa mwaka 1964 na Tundu Lissu aliyezaliwa mwaka 1968!

Kuhusu hoja ile ya kutaka Waziri Kawambwa ajiuzulu na asipofanya hivyo watapiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda nasema lengo hilo pia ni ulevi wa madaraka waliyopewa ya uwakilishi wa wananchi bungeni.

Wandhani kuwa kwao ni wabunge basi wana akili kuliko wananchi wengine. Wanafikiri wanajua mambo mengi zaidi kuliko wote wasiokuwa wabunge, ujinga ambao mtu yeyote akiamini hivyo huwa ni mwenzawazimu kichwani.

Nakubaliana kwa asilimia 100 kuwa bunge linaweza kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kama inavyobainishwa katika Ibara ya 53A(1) ya Katiba ya nchi inayosema:

“Bila kuathiri masharti ya ibara ya 51 ya Katiba hii, bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu endapo itatolewa hoja (ya) kupendekeza hivyo na ikapitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii”.

Hata hivyo, Ibara ya 53A(2) ya Katiba ileile inasema bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hiyo, hoja yoyote ya kutaka kupitisha kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bado haiwezi kutolewa endapo ina mapungufu yafuatayo:

(a) Haina uhusiano wowote na utekelezaji wa majukumu ya Waziri Mkuu kwa mujibu wa Ibara ya 52 ya Katiba, na pia kama hakuna madai kwamba amevunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;

(b) Haijapita miezi sita tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo;

(c) Haijapita miezi tisa tangu hoja hiyo pia itolewe bungeni na kukwama kupitishwa na wabunge walio wengi.

Kana kwamba haitoshi, Ibara ya 53A(3) inasema hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bado haiwezi kupitishwa bungeni isipokuwa kama itakidhi mambo yafuatayo:

(a) Itatolewa taarifa ya maandishi kwa Spika iliyotiwa saini na kuungwa mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wote, lakini isipungue angalau siku 14 kabla ya siku iliyokusudiwa kuwasilishwa bungeni;

(b)  Spika atajiridhisha kuwa masharti ya Katiba kwa ajili ya kuwasilishwa kwa hoja hiyo bungeni yote yametimizwa.

Pamoja na hayo, Ibara ya 53A(4) inasema hoja iliyotimiza masharti hayo itawasilishwa bungeni mapema iwezekanavyo na halafu mwisho; kifungu kidogo cha tano kinaeleza: “Hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu itapitishwa tu iwapo inaungwa mkono na wabunge walio wengi” (mwisho wa kunukuu).

Naomba ieleweke kuwa sisemi genge hilo la kina Tundu Lissu, James Mbatia, Augustine Mrema na wenzao haliwezi kujaribu kukidhi matakwa ya Ibara ya 53A(3)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania niliyoitaja. 

Najua litahangaika kutaka kufanya hivyo ili kusaka umaarufu kwa Watanzania wasiojua lolote wala chochote. Litajaribu kuwarubuni wale wasiojua ukweli likitaka wadanganyike kuwa linapigania haki zao, lakini linachotafuta hasa ni sifa tu za uongo, uzushi na malengo ya siasa za kitapeli.

Haiwezekani kwamba serikali iwe inahangaikia kujibu uzushi unaotengenezwa na kikundi cha wabunge wachache wenye uchu wao wa madaraka, wale ambao wametumwa kwenda kuwasemea wananchi bungeni kwa masuala ya kweli na siyo kutunga umbeya na uzandiki.

Hakuna mpiga kura aliyewatuma kwenda kumng’oa Waziri Mkuu au kushinikiza Waziri wa Elimu kuwa lazima ajiuzulu. Waliapa kuwatumikia Watanzania wote kwa uaminifu ambao ni pamoja na Mizengo Pinda, Dk. Kawambwa na wengineo na kamwe hakuna hata mmoja aliyeagiza kwamba wakifika bungeni kazi yao kubwa iwe ni kutoka nje ya vikao. 

Hakuna mwananchi aliyewatuma wakalazimishe kuwa hoja zao hata kama za uongo na uzushi ni lazima zitekelezwe kwa jinsi wanavyotaka wao, na kwamba zikipingwa ama kutolewa majibu na serikali basi iwe ni nongwa na kususia kama watoto wenye gubu kwa mama wa kambo.

Shinikizo la kutaka kuwang’oa mawaziri fulani kila wanapokwenda bungeni ni siasa zilizotengenezwa kwa chuki na wivu. Haiwezekani nchi yetu iwe na utamaduni kwamba kila kikao cha bunge akang’olewe waziri mmoja, wawili, watatu ama vinginevyo na pale inaposhindikana basi anatishiwa Waziri Mkuu.

Katika kikao kile cha Aprili, 2012, wabunge hao wa upinzani walijiorodhesha majina wakiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe wakitaka eti Waziri Mkuu Pinda ang’oke madarakani. 

Walifanya hivyo wakishinikiza kuondolewa kwa mawaziri sita ambao kwanza; Kamati ya Wabunge Wote wa CCM ilishauri kuwa wawajibishwe kisiasa siyo kwa sababu walifanya kosa lolote, jambo ambalo halina tatizo katika uongozi na utendaji serikalini.

Alipopata taarifa hizo kutoka kwa rafiki zake ambao ni baadhi ya wabunge wa CCM, Zitto alitaka palepale kuwa mawaziri hao wang’olewe “mara moja” utadhani wahalifu wa jinai. Akasema wasipotoka basi wapinzani wangepiga kura ya kukosa imani na Waziri Mkuu na hivyo yeye ndiye abebe msalaba wao.

Licha ya kuanza kujiorodhesha majina kwa mbunge huyo mwenyewe kukimbilia alfajiri katika lango la wabunge kuingia ukumbini ili kuwataka watie saini azimio hilo la hila, kanuni za bunge zilisababisha mpango huo mzima uyeyuke papo hapo utadhani tonge la siagi lililotumbukizwa motoni.

Akitekeleza ushauri wa busara wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko katika baraza hilo ilipofika Mei 7, 2012. Aliwapumzisha baadhi ya mawaziri huku wengine wakibadilishwa wizara na hata vinginevyo na hivyo kuzima hoja hiyo kwa hekima.

Lakini ilipopita miezi miwili tena baadaye, wabunge hao wa upinzani pamoja na wachache wa CCM wanaokuwa na chuki zao wenyewe wakaibuka na jambo jingine. Sasa wakataka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliackim Maswi eti wafukuzwe.

Muhongo aliyekuwa ndiyo kwanza amemaliza mwezi mmoja tu katika wizara hiyo akiwa na wadhifa huo alijengewa tuhuma za majungu, wivu, hasira na chuki za maslahi ya kisiasa na hata kiuchumi na kuanza kushinikizwa aondoke.

Naishukuru serikali hasa Rais Kikwete kwa kusema “hatoki mtu yeyote”. Aligoma kwa namna zote kuwang’oa madarakani au kuwahamishia mahali pengine. Namshukuru kwa kutosikiliza majungu yaliyotengenezwa na wabunge hao wenye chuki zao kwa CCM na serikali yake.

Mbali na kutaka Dk. Kawambwa ang’olewe katika mpango huo wa sasa, wabunge hao pia wanapanga kuwang’oa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai kwa tuhuma za kusitisha hoja ya kutaka suala zima la gesi iliyoibua vurugu kubwa kule Mtwara kuwa lijadiliwe bungeni. 

Baada ya awali Spika kusema kuwa angeunda Tume ya Bunge ili kwenda katika mkoa huo kupata ukweli, lakini alitangaza tena baadaye kwamba asingefanya hivyo kwa vile tayari Waziri Mkuu alikuwa amelishughulikia jambo hilo kwa namna zote na kupata suluhu yake.

Mbali na hayo, nani asiyejua ukweli kuwa wao ndio waliongoza uchochezi wote wa gesi ili kukidhi matakwa yao ya kutaka Tanzania isitawalike mwaka 2013? Nani hakumsikia kwa namna moja ama nyingine Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa aliposema kazi hiyo imefanywa na chama chake, na kwamba itaendelea mpaka mwaka 2015?

Leo wanapong’ang’ania iundwe tume ya uchunguzi pamoja na kutaka kulijadili suala hilo bungeni wanadhani kuwa nani hajui lolote wala chochote? Kwa nini serikali ipoteze fedha kwa kuwalipa wabunge waliotarajiwa kuwemo katika kikundi hicho wakati tayari undani na ukweli wa vurugu hizo zote umeshapatikana?

Mgogoro wa Mtwara uliratibiwa na wapinzani haohao kutoka vyama vinane vya siasa ambavyo ni pamoja na NCCR – Mageuzi ya Mbatia, TLP ya Mrema na pia Chadema ya Tundu Lissu, halafu hivi leo wanajidai kule bungeni kwamba iundwe tume ya kuchunguza uchochezi wao utadhani hawahusiki.

Walifanya hivyo kwa kutaka mwakilishi wao ndani ya tume hiyo ambaye ilikuwa lazima awemo, akakutane na viongozi wa umoja wa vyama vyao waliokuwa wakiratibu moja kwa moja uchochezi wao katika mkoa huo, kisha akisharudi Dodoma aje awape mrejesho. 

Walitaka awemo ili akakutane na Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama hivyo wilayani Mtwara, Uledi Abdallah pamoja na Katibu wake, Saidi Kulaga na hivyo kupata undani na ukweli wa sakata lote ili ikiwezekana walitengenezee uongo mpya ama pengine wahamie mkoa mwingine.

Nahitimisha kwa kuuliza swali moja kuwa je; hivi wabunge hawa wenye kazi kubwa ya kuchochea uasi kwa serikali, kupotosha ukweli na kususia vikao vya bunge wana faida gani kwa taifa kama siyo laana?

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

This entry was posted in

2 Responses so far.

  1. Hakuna mwanaume changudoa kama Charles Charles kihiyo aliyeghushi cheti cha fomu four. Jamaa anaendekeza njaa kujifanya mwandishi wa habari wakati si chochote si lolote bali njaa. Mbona hasemi ukweli kuwa alikuwa mwanachama wa CHADEMA? Kijana huyu mwana haramu asiye na baba anakera Mungu anajua. Charles acha uchangudoa uanze kufikiri kuishi bila kutegemea uongo, kughushi, unafiki na kujikomba kama changudoa.

  2. Hakuna mwanaume changudoa kama Charles Charles kihiyo aliyeghushi cheti cha fomu four. Jamaa anaendekeza njaa kujifanya mwandishi wa habari wakati si chochote si lolote bali njaa. Mbona hasemi ukweli kuwa alikuwa mwanachama wa CHADEMA? Kijana huyu mwana haramu asiye na baba anakera Mungu anajua. Charles acha uchangudoa uanze kufikiri kuishi bila kutegemea uongo, kughushi, unafiki na kujikomba kama changudoa.

Leave a Reply