Lema anapiga marufuku
wananchi kupata habari?
o Heche naye aonyesha anavyotumiwa na Dk. Slaa
Na Charles Charles
MBUNGE wa Arusha Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema amewalisha kiapo wafuasi wake cha kuwapiga marufuku kununua baadhi ya magazeti, kutazama vituo viwili vya televisheni na kutosikiliza kituo kimoja cha redio nchini.
Lema aliyekuwa akiwahutubia wafuasi wake hao kwenye Uwanja wa Kituo cha Mabasi cha Nduruma mjini humo, Jumamosi iliyopita, alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu, kabla ya kurudishiwa na Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam, siku moja kabla ya hapo.
Katika hotuba yake hiyo, Lema aliwaambia wananchi waliokuwepo katika mkutano wake huo kwamba wasinunue magazeti ya UHURU, HABARI LEO, TAZAMA TANZANIA na JAMBO LEO, na kwamba wasiangalie kwa namna yoyote ile vipindi vinavyorushwa na Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) pamoja na Star TV wala kusikiliza kituo cha Radio Five ya jijini Arusha.
Alisema kuwa magazeti hayo sambamba na vituo hivyo vitatu katika ujumla wake vimekuwa vikiisakama sana kihabari Chadema, jambo alilodai kwamba haviitakii mema isipokuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na adhabu yake iwe ni kususiwa kununuliwa, kuangaliwa na hata kusikilizwa kwa namna zote.
Sikutarajia kuwa mbunge na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama na hasa kinachodai siku zote kwamba kinapigania uhuru wa habari, uhuru wa mtu kushirikiana na watu wengine, uhuru wa kutoa maoni, haki ya kupata ujira wa haki pamoja na haki ya kumiliki mali ndiye anakuwa wa kwanza kuwanyima haki hizo zote wapiga kura wake.
Ibara ya 18(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Toleo la 2005 inayoendelea kutumika sasa inaeleza ifuatavyo:
“Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii” (mwisho wa kunukuu).
Akiwa Mbunge na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Lema alipaswa kuwa mstari wa mbele kwa juhudi na maarifa yake yote, kuhakikisha kwamba ibara hiyo ya Katiba ya nchi inaheshimiwa na kila Mtanzania, lakini inashangaza kuona badala ya kuitetea kwa nguvu zake zote, yeye ndiye anakuwa wa kwanza kuikiuka kwa kuwataka watu wavibague baadhi ya magazeti, redio na televisheni nchini ili wakose habari.
Ni ajabu kuona mbunge anakuwa na kinyongo na baadhi ya vyombo hivyo vya habari eti kwa sababu tu haviimbi utukufu wake kama vinavyofanya vile ‘vinavyomilikiwa’ kwa namna moja ama nyingine na chama chake, jambo ambalo ni ujinga kuvilazimisha vyote viwe kama midomo yake au kumsifu kila kwa kila neno analosema kinywani mwake hata kama halina faida yoyote kwa watu wengine, taifa letu, Afrika yetu au hata ulimwengu.
Ni ujinga kutaka eti magazeti yote, redio pamoja na vituo vyote vya televisheni nchini kila moja iwe inatangaza mambo anayoyataka mwenyewe au kuwaponda wengine, na kwamba kila anapowatukana wanachama, viongozi na wafuasi wa chama kilichopo madarakani ama serikali yake basi vyote vimuunge mkono katika hali anayoitaka yeye.
Bila ya kujali itikadi yake ya kisiasa na kuiona kuwa ni bora kuliko zote zilizobaki, Lema anapaswa aheshimu ukweli kwamba kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na kueleza fikra zake kwa watu wengine, jambo ambalo linaelezwa vizuri katika Ibara ya 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anapaswa akubali na kuheshimu ukweli kwamba kila mtu ana haki ya kuamini chama cha siasa anachokitaka yeye mwenyewe, ile ambayo imeelezwa katika Ibara ya 3(1) ya Katiba hiyo ya nchi inayosema ifuatavyo:
“Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, (na) yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa” (mwisho wa kunukuu).
Katika hali hiyo na hata vinginevyo, hatua iliyofanywa na Lema ya kuwalisha yamini wafuasi wake kuwa wasinunue magazeti ya UHURU, HABARI LEO, TAZAMA TANZANIA na JAMBO LEO, kutosikiliza kituo cha Radio Five wala kutoangalia Star TV na TBC1 ni ujinga uliovuka mpaka akilini.
Yeye mwenyewe anafahamu yamini yake kwa wafuasi wake siyo lolote wala chochote na hakuna yeyote anayeweza kuwa vyovyote pindi akienda kinyume chake.
Haiwezi kumdhuru yeyote hata iweje kwa sababu siyo Mungu wala taasisi ya kisheria. Ana mfano hai kuwa hata yamini aliyokula Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa kwa Mungu wake siku alipotunukiwa ushemasi na upadri alikuja kwenda kinyume chake, lakini bado hakufanywa chochote.
Alimwahidi Mungu kwamba angeishi kiseja katika maisha yake yote, lakini akashindwa na kufunga ndoa na mwanamke wakati akiwa Mtawa wa Kanisa Katoliki, yule aliyepata naye watoto wawili na hatimaye akawatelekeza mkoani Manyara.
Wote waliokula kiapo hicho mkutanoni siku hiyo kwamba hawatanunua kabisa magazeti hayo, hawataangalia vituo hivyo viwili vya televisheni wala kusikiliza kituo hicho cha redio hakuna hata mmoja ambaye kweli ataacha kwa kumhofia Lema isipokuwa kama pia ni mjinga wa kufikiri kichwani.
Pamoja na sababu nyingine, wengi waliapa kwa kuogopa macho ya watu ili kuepuka vipigo vya baadhi ya wafuasi wake ambao kuna wengine ni wendawazaimu vichwani kama yeye mwenyewe, lakini walipofika majumbani wakaendelea kuzingalia TV zote hizo zikiwemo taarifa zake za habari, na pia kuna wengine waliendelea kusikiliza Radio Five na kusoma magazeti yote hayo kwa namna moja ama nyingine.
Mbali na kuzuia uhuru wa kupewa taarifa za matukio ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli nyingine za watu, kiapo kilichotolewa na Lema kwa wafuasi wake pia kililenga kuzuia ajira kwa baadhi ya vijana wanaoishi, kutunza familia na kutoa huduma mbalimbali kwa wategemezi wao kwa kufanya biashara ya kuuza magazeti hayo bila ya kujali itikadi zao za kisiasa.
Hatua yoyote ya kuwalisha watu kiapo kwamba wasiyasome maana yake ni kutaka vijana hao washindwe kuwahudumia wake zao, waume zao, watoto wao, baba zao, mama zao, babu zao, bibi zao, watumishi wao wa ndani na hata kutoa msaada wowote kwa ndugu zao wengine na kadhalika.
Anataka wakose ajira ili pengine wawe wezi wa mifukoni, vibaka wa usiku, matapeli wa mjini, majambazi wanaoua watu, makahaba wanaouza miili yao kwa kutoa mapenzi ya kawaida au kinyume cha maumbile yao na kufanya uhalifu mwingine.
Badala ya kuzungumzia ujinga na kuwalisha watu viapo vya kiwendawazimu mkutanoni, Lema alipaswa angalau ajibu tuhuma za jinai zinazoelekezwa kwake hivi sasa na baadhi ya vyombo vya habari zikiwemo za wizi wa kuaminika, ufisadi wa mali na misaada ya fedha na mali nyingine kwa chama chake na kutokuwa mwaminifu akiwa kiongozi mwandamizi wa Chadema na mbunge wa kuchaguliwa jimboni.
Likiandika katika toleo lake namba 220 la Jumanne Desemba 11 – 17, 2012, gazeti la FAHAMU litolewalo mara moja kila wiki lilidai kwamba Lema anatuhumiwa kutafuna fedha zilizochangwa na wanachama, viongozi na wafuasi wa Chadema ili kugharamia maandamano na mikutano ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) hata kama inafanyika kwa vurugu, fujo na umwagaji wa damu.
Alipaswa aitumie nafasi hiyo kuwaambia wapiga kura wake endapo anahusika au hahusiki kwa namna moja ama nyingine na tuhuma za ‘kuingia mitini’ na pikipiki aina ya Kawasaki iliyotolewa msaada na wafadhili wa Chadema.
Alipaswa aseme ni wapi alikolipeleka trekta alilokabidhiwa na wafadhili wa Chadema ili kuwasaidia wajane kwenye mashamba yao, pembejeo ya kilimo aliyopewa pindi tu baada ya kuapishwa kwake na kuwa mbunge mpya wa Arusha Mjini mwaka 2010.
Alipaswa awaambie ni wapi lilikokwenda na ilikuwaje, hatua ambayo ingewezesha wajue endapo linafanya kazi aliyoelekezwa na wafadhili waliompa kwa ajili ya wajane hao, kina mama ambao kuna wengine waliachiwa watoto ama pengine wajukuu baada ya kufiwa na wapendwa wao.
Alipaswa awaeleze kuhusu ukweli wa tuhuma dhidi yake kwamba amekuwa akichangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wajane na watoto waliofiwa na wazazi wao na kuzitafuna zote, na kwamba anatumia propaganda zinazolenga kuwadhoofisha baadhi ya wanachama na viongozi wenzake wa Chadema.
Alipaswa ajibu tuhuma kwamba amekuwa akichangisha mamilioni ya fedha kutoka kwa matajiri wa Arusha akidai kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Taifa wa M4C, na kwamba hata fedha zilizochangiwa familia za marehemu waliopigwa risasi siku ya maandamano ya vurugu za Chadema za Januari 5, 2011 hadi sasa hazijawafikia walengwa.
Alipaswa azungumzie tuhuma kwamba amekuwa akikusanya fedha nyingi anazodai kuwa za kusomeshea watoto kupitia Shirika la Arusha Development Fund (ARDF), lakini zote au nyingi kati yake hazifahamiki ni wapi zinakokwenda.
Alipaswa awaambie kuhusu madai kwamba alitumia shirika hilo pia kuombea kiwanja cha ujenzi wa hospitali ya umma, gari la wagonjwa na vifaa vingine vya huduma kwa ajili ya jimbo hilo la Arusha Mjini.
Kukimbilia kuwatisha watu kwa yamini kuwa wasinunue magazeti fulani, wasikilize redio fulani au wasiangalie vituo fulani vya televisheni ni harakati za kijinga au wendawazimu wa kufikiri ambao ni ajabu zaidi unapofanywa na Mbunge, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha siasa na hata kiongozi mwingine yeyote wa umma.
Mbali na Lema, Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche alinikumbusha pia tuhuma zake alipodai kuwa chama hicho kinajipanga kumpeleka Ikulu Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa ifikapo mwaka 2015.
Akiandika katika baadhi ya mitandao ya kijamii wiki iliyopita na baadaye kulithibitishia gazeti dada la MZALENDO, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza alieleza kwa kina namna Heche anavyotumiwa na Dk. Slaa ili kuligawa na kulivuruga baraza hilo la vijana wa Chadema kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Katika kufanya hivyo, Shonza alidai kuwa Dk. Slaa ameidhinisha Heche alipwe mshahara wa shilingi 700,000 kila mwezi kutokana na ruzuku inayotolewa na serikali kwa Chadema, jambo linalokwenda kinyume cha Katiba ya chama hicho kwa sababu anayepaswa kulipwa mshahara namna hiyo ni Katibu Mkuu wa Bavicha na siyo Mwenyekiti wake.
“Kumlipa mshahara Heche ni kuligawa Baraza la Vijana kwa sababu ni ukiukwaji wa Katiba ya chama…Ni wazi (kwamba) anamlipa fadhila kwa yale aliyofanya ya kuendesha baraza kwa misingi ya kauli za Katibu Mkuu”, anasema Shonza katika taarifa yake hiyo na kumshutumu kwa kuingiza ukanda na ukabila ndani ya Chadema.
Mbali na tuhuma za mshahara, Shonza pia anasema Dk. Slaa aliidhinisha kuwa Heche alipwe shilingi 2,000,000 za pango la nyumba aliyotafutiwa na Chadema baada ya kuwa Mwenyekiti wa Bavicha.
Hatua hiyo inatajwa kuwa inawabagua viongozi wa Bavicha kimatabaka ambapo Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na wengine wote hawana umuhimu, na kwamba hawaonekani kuwa lolote wala chochote katika chama hicho na huenda hawana faida yoyote kisiasa.
Mlolongo wa tuhuma hizo pia unagusia gari aina ya Nissan Patrol lenye rangi nyekundu linalodaiwa kutolewa kwa Bavicha na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Tanzania Bara), lakini katika hali ya ufisadi, Makamu Mwenyekiti huyo anasema lilichukuliwa na Heche anayelitumia kwa shughuli zake mwenyewe huku dereva wake akitajwa kuwa ni mdogo wake.
Katika hali hiyo, sishangai hata kidogo kumuona kijana huyo akitangaza mkutanoni kuwa Dk. Slaa ndiye mgombea urais wa Chadema mwaka 2015 kinyume cha Katiba, kanuni na taratibu nyingine za kawaida za kichama.
Anafanya hivyo ili kuthibitisha tuhuma za Shonza dhidi yake kuwa kuna mchezo ‘mchafu’ ambao unaendelea kati yake na Dk. Slaa huku viongozi wengine wa Bavicha wakitengwa.
Wanalipana fadhila kutokana na kazi wanazopeana kwa ajili ya maslahi yao na siyo kwa faida ya chama wala wanachama, viongozi au wafuasi wa Chadema kama taasisi ila kama kampuni binafsi au Shirika Lisilokuwa la Kiserikali (NGO) linalomilikiwa na familia ama watu wenye malengo wanayoyajua wenyewe.
Bila ya kujali kuwa ni ndani ya Chadema na hata vinginevyo sehemu zote duniani, hakuna Mwenyekiti awe wa NGO, chama cha siasa wala taasisi yoyote na hata vitengo vyake anayelipiwa pango la nyumba au kupewa mshahara ila wote wanapata posho za vikao peke yake, safari ama za uwajibikaji pale wanapokuwa katika kazi zinazotajwa na Katiba za taasisi zao.
Hawalipiwi kodi iwe ya pango ama nyingine yoyote wala kupewa mishahara kwa vile kazi zote zinazohusu uenyekiti haziwi za ajira isipokuwa kujitolea, hivyo haiwezekani Heche afanyiwe kinyume chake endapo siyo rushwa ya kisiasa anayopewa ili naye pia ‘amlinde’, amtetee au kumuunga mkono kwa nguvu zake zote Dk. Slaa.
Aliposema kuwa anakusudia kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kama chama chake kitampitisha, Zitto alikemewa kwa nguvu nyingi na viongozi wake waliodai kwamba muda wa kutangaza jambo hilo bado haujafika na hata kukaribia pekee.
Alikaripiwa na mwasisi wa Chadema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa Mstaafu wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei na hata Mwenyekiti wa Taifa sasa, Freeman Mbowe na pia Dk. Slaa kwa ulimi wake mwenyewe.
Kinachonishangaza sana ni ukweli kwamba Zitto hakutangaza kuwa yeye ndiye mgombea urais wa chama hicho wakati huo, badala yake alichosema ni kwamba ataomba ridhaa ya kufanya hivyo kwa kuzingatia Katiba ya Chadema, kisha akaomba Mungu akubaliwe na wenzake ili akiipata nafasi hiyo aitumie vizuri kuiongoza Tanzania kwa jinsi inavyopaswa.
Tofauti na kijana huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa muhula wa pili sasa, Heche yeye ametangaza rasmi kuwa katika uchaguzi huo mkuu ujao, mgombea urais wa Chadema atakuwa ni babu huyo wa Karatu aliyetelekeza mkewe na watoto wake.
Amefanya hivyo kwa sababu huenda ndiyo makubaliano waliyofikia kwamba yeye alipiwe pango la nyumba, apewe mshahara huo mnono kinyume cha Katiba ya Chadema na ahodhi gari lililotolewa na Zitto kwa ajili ya Bavicha, lakini naye katika upande wa pili apambane kikamilifu kuhakikisha kuwa Dk. Slaa ndiye anagombea urais mwaka 2015.
Wamelishana yamini kwamba kila mmoja amtumikie mwenzie, hivyo haishangazi kuwa Heche aliamua kumtangaza hadharani mkutanoni babu huyo wa Karatu kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi huo mkuu wa rais, wabunge na madiwani; halafu haijalishi kama alikwenda kinyume cha Katiba, kanuni na taratibu nyingine za Chadema.
Alifanya hivyo sambamba na Lema ambaye aliwalisha yamini wafuasi wake ili wayasusie magazeti yale, televisheni zile pamoja na redio ile kwa sababu wote ninadhani kuwa akili zao za kisiasa ni za kishamba, kilimbukeni na ovyo, na kwamba inawezekana upeo wao wa kupembua mambo ya utawala na uongozi wa umma ni mdogo sana.
Ndiyo maana licha ya kuwa kwao wote ni Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, lakini akili zao bado ni sawa na za watoto wa chekechea, hatua inayosababisha waseme chochote, wakati wowote na mahali popote bila ya kujali ama kufahamu kwamba athari zake kwao au kwa umma ni kubwa kupindukia!
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa e-mail: mimi.mimi011@yahoo.com