Na Charles Charles
IPOKUWA katika ziara zake za kutafuta wadhamini
200 ili kukidhi matakwa ya kisheria, mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Edward Lowassa aliahidi kuingilia mpaka uhuru wa mahakama nchini.
Akihutubia katika Uwanja wa Nzovwe mjini Mbeya,
Ijumaa iliyopita, Lowassa alisema moja kati ya mambo atakayoyashughulikia kwa
haraka kama atashinda uchaguzi mkuu ujao, ni pamoja na kumwachilia huru Babu
Seya.
Mbali na Mbeya, mgombea huyo wa urais anayeungwa
mkono na vyama vyote vinavyounda kundi linalojiita Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), aliirudia tena kauli yake hiyo siku moja baadaye alipokuwa
katika jiji la Arusha.
"Tukiingia madarakani tutamwachia huru Babu
Seya", alisema, kauli iliyoibua mshangao mkubwa miongoni mwa watu makini
waliokuwa wakimsikiliza uwanjani, na pia ikashangaza wengi waliokuja kuisoma
katika gazeti moja litolewalo kila siku nchini, kesho yake.
Nguza Viking, mwanamuziki mpiga solo, mwimbaji na
mtunzi ambaye ni maarufu zaidi kama Babu Seya, anatumikia kifungo cha maisha
jela katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam tokea mwaka 2004.
Alitiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya
Kisutu, Ilala katika jiji hilo, kisha akahukumiwa kutumikia adhabu hiyo kwa
mujibu wa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya Mwaka 2001.
Hata hivyo, mawakili wake wakiongozwa na Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando walikata rufaa katika Mahakama Kuu
ya Tanzania wakipinga hukumu hiyo kwa madai kuwa hakutendewa haki.
Katika hatua hiyo, Mahakama Kuu iliyosikiliza
rufaa hiyo iliitupilia mbali, hivyo adhabu dhidi yake ikaendelea kama
ilivyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu.
Lakini pia, mawakili wa Babu Seya bado
hawakuridhika, hivyo wakakata tena rufaa katika Mahakama ya Rufani Tanzania,
kule ambako ilisikilizwa na jopo la majaji watatu kama sheria inavyoelekeza.
Hata hivyo, jopo hilo nalo liliridhia hukumu hiyo
dhidi ya Nguza, lakini bado Marando akaonyesha nia ya kuendelea kumpigania
mteja wake huyo.
Katika hatua hiyo, wakili huyo aliomba, kuwa
Mahakama ya Rufani iteue jopo la majaji watano ili waipitie tena adhabu hiyo
akiamini mteja wake huyo alizushiwa tuhuma hizo zote.
Ili kumpa haki yake, mahakama hiyo ilikubaliana
na maombi ya Marando ya kuteua jopo hilo la majaji watano, wale ambao pia
waliridhika pasipo na shaka kuwa hukumu ya kifungo cha maisha dhidi ya Babu
Seya ilikuwa ya haki.
Katika kesi ya msingi dhidi yake na wenae watatu,
wawili kati yao wakifanikiwa kuachiliwa huru baadaye, Babu Seya alituhumiwa
kubaka, kunajisi na kulawiti watoto wadogo, wale ambao kuna wengine walikuwa
na wastani wa miaka 10 tu!
Miaka 11 baada ya hukumu hiyo kutolewa dhidi
yake, mgombea urais anayetaka kuwa kiongozi mkuu wa nchi hii anakuja na ahadi
ya kumwachilia huru mhalifu huyo endapo atashinda uchaguzi mkuu ujao!
Siyo kazi yangu kumwandikia hotuba za kuzungumza
anapokuwa mikutanoni, na pia si jukumu langu kumwelekeza cha kusema hususan
kero au mahitaji ya Watanzania.
Pamoja na hayo na hata vinginevyo, Watanzania
bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, dini zao, makabila yao, rangi za ngozi
zao, kazi zao, maeneo yao, rika zao ama jinsia zao na kadhalika kamwe hawana
hitaji la kutaka kuachiliwa kwa mhalifu yeyote.
Aidha, Watanzania nikiwemo mimi hawahitaji, kwa
namna yoyote ile kuachiliwa kwa mhalifu wa aina ya Babu Seya aliyetiwa
hatiani kwa makosa ya ubakaji, kunajisi au kulawiti hadi watoto wa
miaka 10 tu!
Tumeona maendeleo makubwa kabisa yaliyoletwa na
serikali zilizopita hadi hii ya sasa, zote zikiongozwa kwa makini na viongozi
waliotokana na Chama Cha Mapinduzi, kile ambacho wengi wanakijua kwa kifupi
cha CCM.
Ilianza Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya
uongozi thabiti wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ilifuatia Serikali ya Awamu ya Pili, nayo
ikiongozwa na mwalimu kitaaluma, Alhaji Ali Hassan Mwinyi kuanzia Novemba 5,
1985 hadi Novemba 21, 1995.
Hiyo nayo ilifuatiwa na Serikali ya Awamu ya
Tatu, safari hii ikiongozwa na mwandishi wa habari na mwanadiplomasia,
Benjamin Mkapa aliyekuja kujulikana zaidi kama 'Mzee wa Ukweli na Uwazi'.
Huyo alipong'atuka Novemba 21, 2005 iliingia
madarakani Serikali ya Awamu ya Nne, pia ikiongozwa na mwanadiplomasia
mwingine na afisa mwandamizi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), Luteni Kanali Jakaya Kikwete.
Katika mpangilio wake huo na chini ya viongozi
hao kila moja kwa wakati na enzi zake, serikali zote hizo zilikuja na
mikakati yake ya maendeleo kwa taifa na wananchi wake.
Sitaki kurejea nyuma hadi wakati wa utawala wa
hayati Mwalimu Nyerere, Alhaji Mwinyi au Mkapa, lakini serikali ya sasa,
chini ya Rais Kikwete nayo imefanya mambo mengi makubwa ya maendeleo.
Mfano ni pamoja na mikoa takribani yote nchini
hivi sasa, kwa kiwango kikubwa kabisa kuunganishwa kwa barabara za lami.
Akizungumza katika hafla ya wizara yake ya
kumuaga Rais Kikwete kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam wiki
iliyopita, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli alisema mtandao wa barabara za
lami uliopo hivi sasa nchini ni kilomita 17,700 kutoka chini ya 6,000
zilizokuwepo mwaka 1995.
Mafanikio mengine ni pamoja na ujenzi wa shule za
sekondari kwa kila kata, kupandishwa hadhi kwa hospitali zote za mikoa kuwa
za rufaa, kuongezeka kwa vyuo vikuu ama vyuo vikuu vishiriki na hata kuwepo
kila mkoa nchini na kadhalika.
Pamoja na kusahihisha kidogo kauli yake kuhusu
Babu Seya alipokwenda Arusha, bila shaka baada ya kusutwa na viongozi
wenzake, suala zima la mfungwa huyo, tena aliyetiwa hatiani kwa makosa ya
ubakaji, ulawiti na kunajisi watoto wadogo kabisa kamwe siyo hitaji la
Watanzania wa leo wala wa kesho.
Hata miye nisiyekuwa mwanasheria ninafahamu,
kwamba makosa hayo kwa mhalifu aliyefungwa kwa kuyatenda kamwe hapewi msamaha
wowote ukiwemo wa rais.
Kama siyo udhaifu wa kufikiri kama mgombea urais,
nani kamdanganya Lowassa kuwa hitaji la Watanzania ni kuachiliwa huru Babu
Seya?
Napatikana
kwa Simu Na. 659 220 220 na 0787 088 870