owassa
aliyekuwa fisadi akiwa
CCM
hata Chadema ni yuleyule
Na
Charles Charles
JUMAPILI iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Meja Joseph Butiku aliwashangaa viongozi
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kumkaribisha Waziri Mkuu
aliyejiuzulu kwa kashfa, Edward Lowassa kuwa mwanachama wao.
Aidha, Butiku aliyewahi kuwa Katibu wa
Rais kuanzia mwaka 1965 hadi 1985 wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, aliwashangaa zaidi kwa kumteua Lowassa kuwa mgombea wa kiti cha Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza kwenye mdahalo kuhusu
umuhimu wa maadili katika kuimarisha amani, haki na umoja kuelekea uchaguzi
mkuu ujao, Butiku alisema Lowassa ni kiongozi mwenye tuhuma za siku nyingi za
ufisadi.
Alisema Lowassa na wenzake kadhaa ambao
hakuwataja kwa majina, wamekijengea Chama Cha Mapinduzi (CCM) mazingira ya
'kunuka' kutokana na hulka yao ya kutoridhika, uchu wa madaraka na kutaka
kujitajirisha kwa njia 'chafu" kwa kutumia 'kichaka' cha siasa.
Katika hali hiyo, Butiku alisema Lowassa
na wapambe wake walipaswa kutoka siku nyingi ndani ya CCM.
"Waondoke (na Chadema) wapokeeni
tu. Kama hukubaliani na msimamo wa mwenye nyumba (akimaanisha Katiba, Kanuni na
Taratibu za CCM) unatoka na siyo kuchafua nyumba ya watu", alisema.
Akionyesha kuwa anajua mambo mengi,
Butiku ambaye ni Meja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alisema
pia watu 'wamenunuliwa' , jambo ambalo limefanyika pia kwa vyombo vya habari
ili vifanye kazi ya matajiri hao.
"Tunajua (kwamba) wengi
wamenunuliwa na wanaonunua vyombo vya habari hawafai kupewa (uongozi wa) nchi.
"Wamewanunua (mpaka) vijana wa vyuo
vikuu, wanamwaga fedha kwa vijana wa pikipiki (au bodaboda) hadi wanakanyagana,
kuumizana na kudhalilika. Ni bora walivyoondoka CCM na hata hivyo walivumiliwa
kwa muda mrefu".
Akirejea historia ya tuhuma za ufisadi
dhidi ya Lowassa mwaka 1995, Butiku alifichua kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya
Pili, Ali Hassan Mwinyi ndiye alimshtaki mbunge huyo wa zamani wa Monduli,
Arusha kwa Baba wa Taifa kwamba ni fisadi asiyefaa kuwa rais wa nchi hii.
"Hivi mnajua kuwa aliyemshtaki
Edward (Lowasaa kwa Mwalimu Nyerere) alikuwa Mwinyi, (wakati huo akiwa rais?)
"Unajua nchi hii bado changa sana.
Mambo mengine unayaacha tu ili (Tanzania) isivurugike. Lakini ukiamua kuyasema
mambo ya Edward (yanatisha) na mimi nayajua", alibainisha.
Naam! Hayo siyo maneno yangu ila yanatoka
kinywani mwa Butiku, Katibu wa Rais na Mkuu wa Mkoa Mstaafu aliyeanza kazi
wakati Lowassa akiwa mtoto wa chekechea.
Anaijua Tanzania na misingi yake kama
anavyokijua chumba anacholala nyumbani kwake. Anawajua watu wengi walioanza
kazi wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, mmoja kati yao akiwa ni Edward
Lowassa.
Anaijua vizuri CCM na sababu za kuundwa
kwake kuliko Lowassa aliyekuja baadaye, tena akitokea chuoni kuja kufanya kazi
akiwa hajui lolote wala chochote.
Namshukuru afande wangu Butiku kwa kusema
yale ambayo, kwa namna yoyote ile kama ningeyasema miye wapambe wake wakiwemo
ninaowajua vyema, wengine ni waandishi wa habari wakongwe wangenimwagia kila
aina ya uzushi na matusi.
Nampongeza kwa kuwa amejitosa waziwazi
kusema ukweli anaoujua, ule ambao kwa wengine utakuwa wa shubiri.
Sina sababu ya kuendelea kurejea kile
kilichozungumzwa na Butiku, lakini hotuba yake angalau imeweza kuwafumbua macho
baadhi ya wapambe wakubwa wa Lowassa, wale ambao kuna wengine wanatumika kama
dodoki bila wao kufahamu.
Nimekuwa nikiandika mara kadhaa kuhusu
uovu wa kutafuta urais unaofanywa na Lowassa, wapambe wake ama sasa na viongozi
wa Chadema yenyewe.
Ingawa Butiku mwenyewe hakutaja gazeti,
kituo cha redio au televisheni wala mwandishi wa habari 'aliyenunuliwa', ukweli
kuhusu jambo hilo unajionyesha hata kwa taahira wa akili.
Ijumaa iliyopita kwa mfano, waandishi wa
habari na watangazaji wa baadhi ya vyombo vya habari nchini, walikodiwa ndege
maalum na Lowassa au kwa uwezeshaji wake kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya ili wakaandike
vizuri habari zake za kutafuta wadhamini.
Kutoka huko walipelekwa hadi Arusha,
Mwanza na hatimaye visiwani Zanzibar utadhani ni watumishi wake mwenyewe.
Walipelekwa kwa usafiri huo wa gharama
kubwa zaidi kuliko wote duniani, lakini pili walilipwa pia posho na huenda
walikuwa wakilipiwa hadi malazi yao, chakula na hata vinginevyo.
Inawezekana walifanyiwa hayo yote kwa
sababu, kikubwa anachohitaji Lowassa ni kuzuia baya lake lolote lisiandikwe
wala kutangazwa na chombo chochote kile cha habari.
Wale wanaofahamu kuhusu suala hili
watakuwa na kumbukumbu nzuri, kwamba hata wakati akitafuta wadhamini kwa ajili
ya kuomba uteuzi wa kugombea urais kupitia CCM, Lowassa alikuwa 'akimiliki' na
kuzunguka na timu maalum ya waandishi wa habari.
Alikuwa akizunguka nao kwa magari ya
kifahari aina ya Landcruiser VX, na pia alikuwa akipaa nao kwa ndege kama
ilivyokuwa kutoka Iringa hadi Songea, mkoa wa Ruvuma.
Mtu anayekuchukua kutoka Dar es Salaam
na kuruka naye kwa ndege hadi Mwanza, ukasafiri kwa magari ya kifahari kutoka
huko hadi Geita, Mara, Simiyu, Geita, Shinyanga, Tabora na kadhalika kwa
gharama zake yeye hakika huwezi kuandika maovu yake ila kumpamba hata kwa
uongo.
Haiwezekani akuzungushe kila mkoa huku
akikulipia mahitaji yako yote kama mwanaye, anakulipa mpaka posho ya shilingi
100,000 kila asubuhi na kukukirimu kwa kila kitu halafu uandike maovu yake.
Kama mwandishi wa habari anafanyiwa hayo
yote, halafu anayemkirimu anazunguka naye muda wote inabidi awe na roho ngumu
kama ya paka ndipo aweze kuandika ukweli.
Ndiyo maana wakati wote wa kutafuta
wadhamini ndani ya CCM, waandishi wa habari aliokuwa akizunguka nao hata
siku moja hawakuandika maovu yake.
Walishindwa kuhabarisha kwa mfano namna
watu, katika baadhi ya maeneo walivyokuwa wakigombea au kuhoji posho walizokuwa
wakiahidiwa ili kwenda kumdhamini.
Hakuna aliyeweza kuandika ama kutangaza
jinsi walivyokuwa wakisombwa na malori, tena ya kukodi wakitolewa takribani
kila eneo la mkoa anaokwenda.
Mfano mmojawapo ni Mbeya ambako watu
walisombwa namna hiyo kutoka wilaya zote za mkoa huo ambazo ni Mbarali, Kyela,
Rungwe, Ileje, Momba, Mbozi, Chunya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Wapo waliotoka hadi nje ya Mbeya kwa
kusafirishwa kutoka Rukwa, Njombe na Iringa huku alipokwenda Mwanza wakitolewa
mpaka Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Kagera, Geita, Mara, Manyara, Arusha
na wengine Kilimanjaro.
Pamoja na kusaka 'mafuriko' hayo ya
'kutengeneza', watu wamekuwa wakidanganywa vinginevyo ili 'kumbeba' tajiri huyo
kwa gharama zake.
Kama alivyobainisha Butiku, harakati za
Lowassa za kutaka kwenda Ikulu kwa gharama zozote zimewakumba hadi wanafunzi wa
vyuo vikuu, waendesha bodaboda na makundi mengine kwa kuwalipa mamilioni ya
fedha.
Pamoja na 'uchafu' wote huo
kujulikana hadharani, vyombo kadhaa vya habari kamwe haviandiki au kutangaza
chochote.
Ndiyo maana haishangazi kusikia kuwa
baadhi ya wahariri wa magazeti, vituo vya redio na televisheni nchini wiki
kadhaa zilizopita wamelipwa shilingi 1,000,000 kila mmoja.
Tunaambiwa fedha hizo wamelipwa ili
wazuie taarifa zote za udanganyifu wa Chadema au Lowassa, na pia wahakikishe
chama hicho na mgombea wake huyo wa urais wanapambwa kwa namna zote.
Mimi mwenyewe ni shahidi wa posho hizo
za Lowassa kwa waandishi wa habari.
Niliitwa na kaka yangu huyo mwaka 2011
kwenda ofisini kwake, Mikocheni jijini Dar es Salaam ambako aliniambia, na hapa
ninanukuu:
"Wewe ni mwandishi mzuri wa makala.
Naomba unisaidie kunipamba kwenye magazeti ambapo, kila mwezi utakuwa unakuja
hapa unachukua shilingi 300,000", aliniambia Lowassa kwa kinywa chake
mwenyewe na kuongeza:
"Usiponikuta mimi utakuwa unamkuta
sekretari wangu na atakupa, nitamwelekeza".
Kwa vile isingewezekana ofisini kwake
kumwambia "hapana", kauli yangu kwake ilikuwa ya maneno manne tu:
"Hakuna tatizo Mheshimiwa, nitafanya".
Nilipomwambia hivyo, Lowassa aliinama
chini ambapo, kiasi cha dakika moja hivi baadaye aliinua macho yake na
kunikabidhi shilingi 300,000 taslimu kama mfano, zote zikiwa noti za shilingi
10,000 kila moja.
Nilimpa mkono na kumwambia
"nashukuru sana", lakini baada ya kumuuga na kuondoka sikurudi tena,
na pia sikuwahi kuifanya kazi hiyo hadi leo.
Sikutaka kufanya hivyo kwa jeuri moja tu
ambayo pia nimekuwa nikiisema mara nyingi.
Siwezi 'kununuliwa' na mtu kwa fedha
zake ili nimuunge mkono, nimpambe magazetini au niwe 'mtumwa' wake kwa namna
moja ama nyingine.
Naweza tu kumuunga mkono mtu yeyote kwa
kuangalia hoja zake, sifa zake na uwezo wake wa kazi anayoomba kuifanya na siyo
vinginevyo.
Ndiyo maana sikushangaa nilipopata
habari kuwa baadhi ya wahariri wa magazeti, vituo vya redio na televisheni
nchini wamehongwa shilingi 1,000,000 kila mmoja ili wampambe Lowassa katika
harakati zake za kutaka awe Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Ndiyo maana sikushangaa kusikia Butiku
naye amekemea jambo hili.
Katika hali hiyo na hata vinginevyo,
wale wanaodhani kuwa Lowassa aliyeitwa fisadi alipokuwa CCM, tena kwa kiwango
kikubwa zaidi na viongozi wa Chadema yenyewe atabadilika kwa kwenda katika
chama chao.
Daima atabaki yuleyule na vilevile kama
zamani hata iweje.
Mtu akizoea kula nyama ya nguruwe hawezi
akaacha eti kwa sababu tu amehamia kijiji kingine!
Napatikana
kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244