• CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM CHAMA MAKINI KINACHOFANYA MAAMUZI KWA VIKAO RASMI
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA

UWEZO WA MANGULA








Uwezo wa Mangula umesababisha 
kiwewe kwa Chadema, Kilimwiko
 Na Charles Charles 


 JUMATANO ya Novemba 12, 2012, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mshauri wa Masuala ya Kisiasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Kitila Mkumbo aliendeleza wimbi lake la kutokubaliana na kitu chochote kinachofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wala serikali yake.

Akiandika katika gazeti moja la kila wiki, siku hiyo, Dk. Mkumbo anayetumia kivuli cha uhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufanya siasa zake hizo, alihoji kama Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula ataweza kuimaliza rushwa katika chama hicho akidai takrima ilimshinda.

“Hakuna haja ya kuwakumbusha wasomaji kwamba Philip Mangula alikuwa Katibu Mkuu wa CCM kwa miaka kumi mfululizo katika kipindi chote cha urais wa Benjamin Mkapa. Katika kipindi hiki, rushwa ndani ya CCM ilikuwa ikiitwa takrima na Mangula alikuwa mmoja wa wahalalishaji wakubwa wa rushwa hii”, aliandika katika makala yake hiyo na kuendelea:

“Nikumbushe pia kwamba rushwa kubwa kabisa kuwahi kutokea katika nchi yetu, ule wizi katika Benki Kuu, watuhumiwa wakuu wakiwa ni baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM na serikali yake, maarufu kama EPA ilitokea kipindi ambacho alikuwa Katibu Mkuu wa CCM”. 

Akizidi kubainisha, Dk. Mkumbo anasema hata uuzaji wa nyumba za wafanyakazi wa umma ambao kimsingi ulikuwa ni wizi wa mali ya umma ulitokea kipindi cha Ukatibu Mkuu wa Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM hivi sasa.

Katika hali hiyo, Mshauri huyo wa Chadema anasema kuwa ni upotoshaji na upotoshwaji kujaribu kuamini kwamba rushwa haikuwepo katika miaka 10 ambayo Mangula alikuwa Katibu Mkuu wa CCM bali alishindwa kuidhibiti, hivyo hawezi kuimaliza katika “miaka miwili iliyobaki kabla ya Rais Jakaya Kikwete kustaafu” mwaka 2015.

“Pengine tumkumbushe pia Mangula kwamba kilichomponza hadi akashindwa kuwa Mwenyekiti (wa CCM) wa Mkoa wa Iringa mwaka 2007 na kushindwa kupata ujumbe wa NEC (au Halmashauri Kuu ya Taifa), tena katika wilaya mpya huko Njombe ni mahubiri yake ya uadilifu”, anasisitiza.

Mbali na kiongozi huyo wa Chadema, mmoja kati ya waandishi wa habari wa siku nyingi hapa nchini, Lawrence Kilimwiko naye aliandika makala nyingine siku ileile katika gazeti moja la kila siku, ile iliyokuwa na kichwa kinachosema “Kufufuka kisiasa kwa Mangula na hatima ya CCM”.

Pamoja na mambo mengine, Kilimwiko alidai kuwa Mangula aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM wakati wa uongozi wa Rais Benjamin Mkapa katika chama hicho, alitoswa “kiaina” alipoingia madarakani Rais Kikwete.

Anasema hata kushindwa kwake katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa kulitokana na kupinga rushwa, nafasi ambayo ilinyakuliwa na mwanachama “mwenye elimu ya ngumbaru” kwa maana ya Mbunge wa Njombe Kaskazini, Deo Sanga.

Anaonyesha wasiwasi mkubwa endapo Mangula atafanikiwa akidai chama hicho sasa kimezungukwa na wafanyabiashara za kisiasa waliofahamika katika miaka iliyopita kama wanyonyaji, kupe, wabaguzi, wanyanyasaji na wakandamizaji.

Hao “ndio waliohodhi madaraka ya chama na serikali na kuwageuza raia kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao. Wahujumu uchumi waliotengwa enzi za Azimio la Arusha ndio (ambao hivi) sasa wamegeuzwa wafadhili wa chama ambacho Mangula ni Makamu Mwenyekiti”, aliandika.

Anasema huko nyuma, CCM ilisimamia maslahi ya wakulima na wafanyakazi, na kwamba ilitarajiwa kuendeleza mapambano dhidi ya unyonyaji, dhuluma, uonevu, ujinga, maradhi na umasikini.

“Je, Mangula ataweza kuongoza chama ambacho nguvu ya pesa inanunua madaraka na madaraka yananunua uongozi? Ataweza kurejesha heshima na haiba ya CCM iliyopotea miongoni mwa Watanzania? Jibu ni hapana”, anaandika, kuhoji na kutoa jibu mwenyewe.

Namheshimu Dk. Mkumbo kama Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini sikubaliani naye kwa namna zote anapoigeuza nafasi hiyo kuwa ‘hirizi’ ya kuijenga kisiasa Chadema, kuwapotosha watu na kuwadhalilisha viongozi wa CCM na serikali yake.

Sikubaliani na Kilimwiko anapotumia uandishi wake wa habari wa siku nyingi kuwa ‘kichaka’ cha kukidhia matakwa yake ya kisiasa, kuwadanganya wasomaji wake na kupotosha kwa makusudi kuhusu undani na ukweli wa CCM. 

Nashangazwa na madai yao kwa Mangula kwa sababu yanalenga kumshushia hadhi yake, kumvunjia heshima yake, kumvunja moyo ili akate tamaa na kutaka kumdhalilisha nje na ndani ya chama chake.

Wanalenga kumkejeli Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Jakaya Kikwete aliyependekeza jina la Mangula kwamba agombee nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara) na kushinda kwa kutaka aonekane siyo kiongozi makini, mweledi na hata mwenye maono.

Ni uongo kwa mfano kudai katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa nafasi ya Mwernyekiti wa Chama hicho wa mkoa wa Iringa mwaka 2007, Mangula alishindwa kwa vile hakutoa rushwa, hivyo wanachofanya ni kutaka kumwaibisha Deo Sanga kwamba hakushinda kwa haki ila alihonga.

Wanasema uongo kwamba ili mgombea ashinde katika chaguzi zote za CCM ni lazima atoe rushwa, vinginevyo hata iweje hawezi kabisa kushinda wakati ni demokrasia ila inaonekana ajabu kwa sababu haipo katika vyama kama Chadema.

Huko ni lazima mshindi awe mwenye madaraka au aliyewahi kushika cheo kikubwa kuliko wote anaogombea nao, vinginevyo watalazimishwa kuyatoa majina yao kama Zitto Kabwe alivyoshinikizwa ampishe Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema aliyekuwa akimaliza muda wake mwaka 2009, Freeman Mbowe. 

Ndivyo inavyokuwa mpaka katika ngazi za chini kabisa. Ndiyo maana hata mwaka 2010, wagombea ubunge walipangwa mezani na viongozi wa kitaifa, nafasi ambazo wenyewe walijigawia kwanza majimbo na kupiga marufuku mtu mwingine kuwapinga kwa namna yoyote.

Wanadhani Sanga au mtu mwingine yeyote hakutakiwa kupambana na Mangula eti kwa sababu tu alikuwa ni Katibu Mkuu, udikteta ambao katika CCM haupo na hautakuwepo hata baadaye.

Kuhusu kigezo cha elimu, Ibara ya 14(3) ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 1977 inasema kila mwanachama ana “haki ya kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi wa CCM na ya kuchagua viongozi wake kwa mujibu wa Katiba na Taratibu za CCM”.

Wapi panasema kuwa lazima mgombea ahitimu kiwango kipi cha elimu ndipo agombee uongozi? Ni mahali gani pameweka ubaguzi kama alivyodai Kilimwiko kwa kuonyesha kuwa Sanga hakustahili kugombea?

Ni ufinyu wa kufikiri au ni kasumba kutaka kuwabagua watu waliokosa bahati ya kusoma angalau hadi sekondari, taasisi nyingine au vyuo vikuu ili wasipewe fursa yoyote ile ya uongozi hata kama wanafaa kuliko wasomi wa sampuli ya Kilimwiko.

Wanataka nafasi zote zihodhiwe na wachache waliosoma mpaka vyuo vikuu ama taasisi nyingine na kupata vyeti au diploma, lakini waliokosa nafasi hizo hata kama wananchi wanaridhika nao wazuiliwe kuongoza.

Wamekazania kutolea mfano huo wa Sanga aliyeishia darasa la saba huku wakidhani kuwa uhadhiri wa chuo kikuu na uandishi wa habari ni kuelewa kila kitu, jambo ambalo ni ujinga wa kufikiri unapoona mtu akiwadharau wenzake.

Wanampakazia Deo Sanga kwa chuki zao kwamba hakusoma kabisa shuleni isipokuwa ana “elimu ya watu wazima”, uongo ambao inayolengwa zaidi ni CCM wakidhani kuwa kusoma mpaka chuo kikuu ndiko kuelimika wakati ambapo siyo kweli. 

Kama elimu ndicho kigezo mama cha mtu kupata uongozi, kwa nini hawakipondi chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini ambacho Mwenyekiti wake wa Taifa, Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo hakusoma hata elimu ya chekechea?

Mbona hawaitolei mfano Afrika Kusini kuwa inaongozwa na Rais ambaye hana hata elimu hiyo ndogo ya ngumbaru, lakini imeendelea kushinda nchi zote Afrika katika nyanja zote zikiwemo ambazo ni muhimu zaidi za uchumi na kijeshi?

Kwa nini hawasemi Zimbabwe ina hali gani wakati Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha Zimbabwe African National Union – Patrotic Front (ZANU – PF) kinachotawala, Robert Mugabe ndiye Rais aliyesoma kuliko wakuu wote wa nchi zote duniani akiwa na shahada saba za vyuo vikuu?

Kwa nini Zimbabwe haijatulia ikilinganishwa na Iringa iliyokuwa chini ya Sanga akiwa Mwenyekiti wa Chama kilichopo madarakani katika miaka yote mitano ya uongozi wake?

Akiwatunukia shahada wahitimu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Ghana mjini Accra mwaka 1958, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, hayati Osagyefo Dk. Kwame Nkrumah alisema: “Hakuna kitu kibaya kabisa duniani kama cha mtu kujifanya kwamba amesoma kuliko wengine. Elimu inatufanya tuwe wapole na wanyenyekevu, nje ya hapo ni wendawazimu”.

Nikirudi kwa Mangula, ni uongo na uzushi uliopitiliza kudai kwamba alipokuwa Katibu Mkuu wa CCM ndipo rushwa ilipoanza ama ilishamiri hapa nchini.

Akiongea na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Simba Grill, Kilimanjaro Hotel ambayo sasa inaitwa Kilimanjaro Kempisyk Hotel jijini Dar es Salaam Machi 25, 1995, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzamia, hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema:

“Siyo kwamba wakati wa (utawala wa) Serikali ya Awamu ya Kwanza rushwa haikuwepo hapa nchini bali ilikuwepo” (mwisho wa kunukuu).

Nani alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha Tanganyika African National Union au TANU kilichokuwa madarakani wakati huo, kile ambacho kilipoungana na Afro-Shiraz Party (ASP) cha Zanzibar na kuwa CCM hadi mwaka 1996 alipoteuliwa Mangula kushika nafasi hiyo huku rushwa ikiwepo?

Nani aliyelifahamu zaidi tatizo hilo kati ya Kilimwiko, Mkumbo na hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa Rais wa Tanzania kwa miaka 23 mfululizo? 

Nani angeweza kulielezea vizuri zaidi janga hilo kati ya hayati Baba wa Taifa, Kilimwiko na Dk. Mkumbo aliyezaliwa mwaka 1971 ikiwa ni miaka 10 baada ya Uhuru wa nchi hii? 

Kana kwamba haitoshi, suala linalohusu kuuzwa kwa nyumba za serikali wakati ambao Mangula alikuwa ni Katibu Mkuu wa CCM nalo halimhusu kwa namna zote.

Hahusiki kwa sababu liliamuliwa na Baraza la Mawaziri ambalo yeye hakuwa mjumbe, hivyo wanaoweza kunyoshewa kidole chochote kile ni Rais Benjamin Mkapa, aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye; aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na pia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na siyo Mangula.

Kama nyumba hizo zingekuwa zimeuzwa kwa maelekezo yoyote ya CCM hapo Mangula angehusika moja kwa moja. Ni dhahiri angehusika kwa vile ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, lakini kwa sababu halikujadiliwa kwa namna yoyote ile na chama hicho inakuwa wendawazimu wa kufikiri kutaka kumhusisha nalo.

Ndivyo pia ilivyo ujinga kumhusisha na wizi wa fedha za EPA katika Benki Kuu wakati hajawahi kuwa Gavana wa BoT, Waziri wa Fedha wala mfanyakazi wa ngazi yoyote wa benki hiyo au Wizara ya Fedha.

Ni ujinga maana wizi huo haukufanyika kwa agizo lake wala la CCM, na pia haukutokana na azimio lolote la kisiasa kutoka chama hicho ambacho Mangula alikuwa ndiye mtendaji wake mkuu.

Ni uongo mwingine mkubwa kusema baadhi ya watuhumiwa katika wizi huo ni viongozi waandamizi wa CCM. Ni uzushi na uzandiki maana hata Dk. Mkumbo mwenyewe akiitwa na kuulizwa ni kiongozi yupi mwandamizi wa CCM aliyehusika na wizi huo anayeweza kumtaja ni aliyekuwa Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM wa Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda.

Lakini akiulizwa kama tuhuma za kumtelekeza mkewe alizonazo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa zinakihusu chama hicho atabaki ‘anajiumauma’ kama mtoto wa kambo. 

Kuhusika kwa Maranda katika kashfa hiyo tayari kamwe hakuwezi kuhusishwa na CCM wala Mangula, lakini kwa muungwana yeyote bado hawezi kuzungumzia suala hilo kwa vile tayari alishatiwa hatiani kuanzia mwaka jana mpaka Alhamisi wiki hii.

Kuhusu kushindwa katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM katika moja kati ya wilaya za mkoa mpya wa Njombe, madai hayo kama mengine pia ni uzushi, uongo, umbeya na uzandiki uliokosa hata aibu ya kudanganyia watu.

Mangula anayetoka katika kijiji cha Imalinyi, wilaya mpya ya Wanging’ombe siyo tu hakugombea ujumbe wa NEC, lakini pia hakugombea hata ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa, Wilaya, Kata wala ya tawi lake la Imalinyi.

Tofauti na uongo huo wa Dk. Mkumbo, wana CCM waliogombea ujumbe wa NEC katika wilaya ya Wanging’ombe na miaka yao kwenye mabano ni Yono Kevela (49), Nebahad Msigwa (32) na Julieth Kadodo (50), mwanamke ambaye pia ni Katibu Muhtasi wa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Iringa Mjini.

Aidha, Kilimwiko katika upande wake naye bado ni mhafidhina wa kufikiri. Anashindwa kufahamu kuwa hata wakati wake alipokuwa mwandishi wa habari wa kawaida na sasa ni vipindi viwili tofauti.

Leo kwa mfano uandishi wa habari umekuwa wa ushindani mkubwa kuliko enzi zake, zile ambazo walikuwa wakisubiri kuitwa na viongozi ili wakapewe taarifa, jambo ambalo sasa hata kwa vijarida vya shuleni peke yake haliwezkani.

Anataka CCM iendelee na siasa za kizamani zilizoishia mwaka 1989 wakati uliokuwa Muungano wa Jamhuri za Kisovieti za Urusi (USSR) uliposambaratika. Anataka iwafungie milango wafanyabiashara kwa vile huenda hajui kuwa uongozi duniani kote umebadilika. 

Anataka CCM iwabague wafanyabiashara huku Chadema ikiwaambia wamiminike kwa wingi na kuwazawadia uongozi kama akina Philemon Ndesamburo, Saidi Amour Arfi na kufadhiliwa kwa kiwango kikubwa na matajiri kama Mustafa Sabodo.

Kwake watu hao wanapokuwa ni viongozi katika vyama vingine au kuvifadhili kifedha ni halali isipokuwa uharamu wao ni pale wanapofanya hivyo kwa CCM. Hapo ndipo anapotaka eti waitwe kuwa wanyonyaji na kupe, wabaguzi na watu wanaohodhi madaraka ya kisiasa na ndani ya serikali.

Anawapotosha wasomaji wake kuwa CCM imeacha kupambana na uonevu, unyonyaji, dhuluma, ujinga, maradhi na umasikini utadhani serikali hivi sasa imefuta Jeshi la Polisi, Idara ya Mahakama na Jeshi la Magareza ili watu waonewe, wadhulumiwe na kukosa wapi wakaseme au wakafungue mashtaka na hata vinginevyo.

Anadanganya hivyo huku akiona idadi kubwa ya shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu vikizidi kujengwa nchi nzima ili kufuta ujinga. Anadanganya eti kuwa CCM haipambani na maradhi huku akiona zahanati, vituo vya afya na hospitali vinavyojengwa kila kona huku madaktari, wafamasia, wauguzi, waganga wasaidizi na wataalamu wengine wa sekta ya afya nchini wakiendelea kusomeshwa kwa wingi.

Anaandika uzushi kuwa CCM imeacha kabisa kupambana na umasikini huku akijionea jinsi gani benki zinavyofunguliwa kwa wingi. Anajua ni namna gani serikali inaongeza bajeti ya Mkakati wa Kuzuia na Kupambana na Umasikini Tanzania (MKUKUTA), na pia anajionea Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) vinavyozidi kuenea kila mahali kuanzia mijini mpaka vijijini.

Watu wasiokuwa na woga wa kudanganya hadharani kama Lawrence Kilimwiko kamwe hawaoni taabu yoyote kusema uongo. Ndiyo maana anadai Mangula amerudi kukiongoza chama kilichopoteza heshima na hata haiba kwa Watanzania!

Anakuja na madai hiyo bila ya kuonyesha ushahidi wala kielelezo chochote, lakini kitu cha ajabu zaidi anakuja na maelezo hayo huku akifahamu kuwa wiki tatu zilizopita, chama anachodai kimepoteza haiba yake kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi mdogo wa viti vya udiwani dhidi ya vyama ambavyo kwake vina mvuto.

Kilishinda kata 22 kati ya 29 zilizoshiriki katika uchaguzi huo huku viongozi wake wapya wakiwa hawakufanya kampeni kama ilivyokuwa kwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu wake, Dk. Wilbroad Slaa; Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, Wakuu wa Idara zote za Makao Makuu jijini Dar es Salaam na wabunge takribani wote.

Inawezekana Dk. Mkumbo, viongozi wenzake wa Chadema na Kilimwiko wameingiwa kiwewe, hatua iliyokuja baada ya Mangula kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM na hivyo kutishwa na uwezo wake mkubwa!

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

This entry was posted in

One Response so far.

  1. Hakuna mwanaume changudoa kama Charles Charles kihiyo aliyeghushi cheti cha fomu four. Jamaa anaendekeza njaa kujifanya mwandishi wa habari wakati si chochote si lolote bali njaa. Mbona hasemi ukweli kuwa alikuwa mwanachama wa CHADEMA? Kijana huyu mwana haramu asiye na baba anakera Mungu anajua. Charles acha uchangudoa uanze kufikiri kuishi bila kutegemea uongo, kughushi, unafiki na kujikomba kama changudoa.

Leave a Reply