• CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM CHAMA MAKINI KINACHOFANYA MAAMUZI KWA VIKAO RASMI
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    MWENYEKITI WA CCM, RAIS JAKAYA KIKWETE AKIWA NA WAJUMBE WA NEC, 25/9/2012, KABLA YA KIKAO KILICHOFANYIKA MJINI DODOMA, KUTEUA WAGOMBEA WA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA. PICHA: BASHIR NKOROMO
  • CHAMA CHA MAPINDUZI

    CCM NDICHO CHAMA CHA SIASA KINACHOONGOZA KWA KUWA NA WAFUASI WENGI TANZANIA

AROBAINI YA CHADEMA









Na Charles Charles

“KUZUNGUKA huku na huko kwa CCM ni kutuiga sisi. Tumeanza muda mrefu baada tu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010”, ndivyo anavyosema Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.

Anaongeza kwamba “Chadema ni mwalimu” huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa mwanafunzi anayefuata nyayo kwa mambo yanayofanywa na chama chake hicho. Alikuwa akizungumza na gazeti moja la kila siku nchini kufuatia ziara iliyofanywa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa CCM, Kanali Abdulrahman Kinana katika mikoa minne ya Arusha, Geita, Mtwara na Rukwa.

Siku chache baadaye, yeye mwenyewe alifanya ziara katika majimbo matatu ya Temeke, Kigamboni na Kinondoni jijini Dar es Salaam na kukumbana na hali ngumu kuliko wakati wote uliopita.

Tatizo hilo liliambatana na ‘kudoda’ kwa harambee ya kuchangia kile kinachoitwa kuwa ni Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) iliyofanyika jijini Mwanza, na kukitia chama hicho hasara ya shilingi milioni tisa.

Wakati hayo yakiendelea, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliibua tuhuma kwa Dk. Slaa kuwa pamoja na kuwashambulia sana viongozi wenzake wilayani Temeke akisema ni mamluki wa CCM, yeye mwenyewe ana kadi ya chama hicho kinachotawala, jambo alilokiri ni kweli na ataendelea kuitunza katika maisha yake yote.

Tayari hali hiyo imeibua mtafaruku katika chama chake ambapo kuna wanachama, viongozi na wafuasi wake hivi sasa hawana tena imani naye na kuanza kumtilia wasiwasi kwa kusema inawezekana pia ndiye anavujisha siri nyingi za Chadema kwa watu wasiohusika.

Wanadai hata siasa zake za vurugu, uchochezi na uvunjaji wa sheria kwa makusudi unalenga kuifanya Chadema ichukiwe na wananchi. Anataka ionekane kuwa inahamasisha umwagaji wa damu, mkakati ambao unafanyika chini kwa chini kwa kisingizio cha M4C ili wananchi  wasigundue.

Nashukuru kwamba hatimaye wengi wameanza kukielewa chama hicho na siasa zake za kitapeli. Wameanza kukitenga wakiwemo viongozi wake waandamizi kama wenyeviti na makatibu wa wilaya, mikoa, madiwani na kadhalika.

Wamo kwa mfano aliyekuwa Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Morogoro, Abel Luanda; aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Morogoro, Rajabu Ali; aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Iramba, Mkumbo; waliokuwa madiwani wa Arusha Mjini ambao ni Rehema Mohammed (Viti Maalum), Frank Takachi (Kata ya Olasiti), Simba Salum (Kata ya Kati) na viongozi wengine lukuki.

Akihutubia mkutano wa hadhara wa CCM kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Rehema alisema wazi kwamba Chadema ni kama kampuni binafsi ya Dk. Slaa na hivyo anaweza kufanya lolote, wakati wowote na mahali popote ili kukidhi matakwa yake mwenyewe kwa kutumia kisingizio chochote.

Alisema amekuwa akitimua viongozi na kuweka wengine jinsi anavyotaka kwa kuwatuhumu kuwa ni mamluki wa CCM, vinginevyo huwatwisha lawama kwamba wanavunja Katiba ya Chadema ambayo hata hivyo haipo matawini, majimboni, wilayani na mikoani isipokuwa kwake mwenyewe.

Ndiyo maana alikwenda akavuruga uteuzi wa mgombea nafasi ya Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza kwa kuwapelekea mgombea ambaye alimteua yeye jijini Dar es Salaam. Aligoma kumtambua diwani aliyegombea kwa njia zote halali, akashinda kura za maoni za ndani ya chama akidai kuwa alishavuliwa uanachama.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Ndago wilayani Iramba wiki tatu zilizopita, Mkumbo alisema ameamua kuacha uenyekiti wa wilaya wa Chadema na kuingia CCM ili apone moyo wake kuliko kuendelea kunyanyaswa kisiasa na viongozi wake wakuu.

Alisema hawezi kuendelea kuwa mwanachama na hata kiongozi wa Chadema katika ngazi yoyote “kwa vile ni chama kilichojaa majungu, fitina na chuki nyingi”.

Madai hayo yanafanana pia na yale yaliyotolewa na aliyekuwa Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Morogoro, Abel Luanda alipohutubia mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini humo.

“Ndani ya Chadema tuliingia kwa bahati mbaya. Ilikuwa kama uko barabarani unasubiri gari na linalotokea unapanda, lakini ukishakuwa ndani unagundua kuwa ni mkweche na kushuka ili usubiri jingine. Tumeshuka na tumepanda gari la kweli linaloitwa CCM”, alisema wakati alipokaribishwa kuzungumza ili kuwawakilisha wenzake wote na kuendelea:

“Nilishikilia chama kizima mkoani, nawahakikishia kuwa hakuna cha maana kinachoendelea kule. Ndani ya Chadema hakuna sera za kumkomboa mlalahoi, badala yake kuna udikteta tu unaofanywa na viongozi wa ngazi za juu”.

Hatua ya kuanza kusambaratika kwa Chadema ilithibitika pia katika ziara ya siku tatu ya Dk. Slaa wilayani Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam. Alikuwa  akiwashutumu viongozi wenzake kuwa ni mamluki wa CCM kwa sababu tu mahudhurio aliyoyakuta huko ni hafifu.

Mathalani, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema wa Jimbo la Kinondoni walimsotesha ukumbini akiwasubiri kuanzia saa 4.00 asubuhi hadi saa 6.47 mchana alipochoka, akafungua kikao hicho na kuzungumza na hao wachache waliofika baada ya wao pia kubembelezwa sana kwa kupigiwa simu zao za mikononi.

Badala ya wajumbe 130 waliotakiwa kuhudhuria ili kujua ni kitu gani wanaambiwa na bosi wao, wale waliofika mkutanoni hadi wakati huo walikuwa chini ya 50 tu huku wakionekana kutokuwa tayari kumsikiliza kwa muda mrefu isipokuwa vinginevyo.

“Chadema ni chama ambacho kinajiandaa kushika dola mwaka 2015, endapo hali hii ya wajumbe kutafutana kwa simu itaendelea ni hatari wakati wa kuunda Baraza la Mawaziri”, alisema na kukiri: “Bila kujipanga wakati huu hakika hali ni ngumu huko tunakokwenda”.

Kama viongozi waliowekwa madarakani ili kukiongoza chama hicho na kuwa kiungo kati ya wanachama, wapiga kura na uongozi wa juu nao tayari wamekichoka; nani atakiunga mkono na ili iweje?

Nimekuwa nawaambia rafiki zangu kuwa tokea mfumo huu wa vyama vingi vya siasa nchini ulipoanza tena mwaka 1992 ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna mpinzani aliyewahi kuwa ‘lulu’ kwa wafuasi wake kama aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha NCCR – Mageuzi, Augustine Mrema.

Aliaminiwa na kuungwa mkono kila mahali mijini na vijijini. Aliteka hisia za wengi kuanzia wazee, kina mama na vijana, matajiri na masikini, wasomi pamoja na makundi mengine.

Ndiyo maana gari lake anapomaliza kuhutubia mikutano ya hadhara hasa mijini kama Dar es Salaam lilikuwa likisukumwa na mamia ya vijana, tena kwa hiari na matakwa yao wenyewe hata kwa zaidi ya saa nzima mpaka wanapokuja kusambaratishwa na polisi waliofanya hivyo ili kumlinda dhidi ya vibaka, wezi na waporaji wengine linapoanza giza.

Lakini alipotamba kwa miaka minne akiwa katika hali hiyo kuanzia mwaka 1995 – 1999, Mrema aligundulika kuwa ni ‘msanii’, muongo, mzushi, mchochezi na mtu anayependa zaidi kusifiwa binafsi akitumia kila aina ya ujanja wa kisiasa kwa kuwadanganya wafuasi wake.

Hapo ndipo umaarufu wake wote uliposambaratika kama kishada kilichokwenda harijojo na kubaki na kikundi kidogo cha watu wenye malengo yao binafsi. Hao bado wanaendelea kumuunga mkono hadi leo na baadhi yao wapo radhi na tayari hata kumfia utadhani kupe linavyong’ang’ania ngozi ya mnyama hususan ng’ombe, mbuzi ama kondoo bila kuiachia hata kama haina damu tena au tayari ameshakufa!

Hivyo ndivyo wanavyofanya wafuasi wa Chadema wakiwemo hadi wasomi, ngumbaru na kadhalika. Wapo ambao pia wamejitokeza kuthibitisha umahiri wao wa kuitetea kwa uongo, uzushi na majungu ya aina zote.

Wanafanya hivyo kwa kupewa matumaini ‘hewa’ na viongozi waandamizi wa chama hicho wakiongozwa na Dk. Slaa mwenye uwezo mkubwa wa ghiliba, uzushi na kufanya kila aina ya siasa za ‘kisanii’.

Wafanya hivyo kwa kusingizia jambo lolote, wakati wowote na mahali popote ili mradi tu wanakidhi matakwa yao wenyewe, watu ambao siku zote wanaishi kwa kutegemea majungu, umbeya na uzandiki wa namna yoyote ile dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), serikali na viongozi wake.

Wamekuwa mahiri wa kuhubiri siasa za kikabila, kikanda na kadhalika kwa kutaka Tanzania itenganishwe kwa utawala wa kimajimbo, ule ambao Mchagga au Mpare kutoka Kilimanjaro hataweza tena kupata uongozi wowote katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Mara au Ruvuma.

Itakuwa marufuku kwa Msukuma kutoka Mwanza, Simiyu, Shinyanga au Tabora kushika uongozi wa ngazi yoyote katika mikoa kama ya Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa, Katavi, Dodoma, Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga na kadhalika.

Hata hivyo hali hiyo imekuwa kinyume baada ya miaka miwili tu ya wanachama, viongozi na wafuasi wa Chadema kudanganywa na kuamini uongo, lakini hivi sasa wameanza kujua ukweli.

Mbali na viongozi waliohama katika mikoa ya Arusha, Singida na Morogoro, watu kama Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Zitto Kabwe naye haelewani kabisa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe kutokana na kila mmoja kutaka ateuliwe yeye kuwa mgombea urais wa chama hicho mwaka 2015.

Mbali na hao, Afisa Mwandamizi wa Kurugenzi ya Sera na Utafiti, Mwita Waitara na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Juliana Sonza nao hawaelewani na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza hilo, John Heche.

Tayari mgogoro huo pia umeanza kuenea nchini ambapo kwa mfano, Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Mbeya, Eddo Mwamalala amesimamishwa uongozi kwa sababu anapinga udikteta, lakini viongozi wa Bavicha wa Mkoa wa Mwanza na sehemu nyingine wanamtaka Dk. Slaa ajiuzulu kwa madai kuwa anakivuruga chama hicho.

Ndiyo maana sasa amechanganyikiwa kiasi cha kupayuka bila mpangilio wowote mdomoni ikiwemo kudai eti CCM inapofanya ziara zake inakuwa inaiiga Chadema, jambo ambalo hata mwendawazimu hawezi kuliamini.

Haiwezekani kwa namna yoyote kuwa viongozi wa CCM ambayo ilianzishwa mwaka 1977 wawe hawajafanya kabisa ziara mpaka walipoiga Chadema wiki tatu zilizopita!

Ndiyo maana Dk. Slaa sasa na ‘vigogo’ wenzake wa kitaifa wamechanganyikiwa baada ya kuanza kususiwa mikutanoni huku viongozi wengine wakisema wamechoshwa na udikteta, kuburuzwa kusikoisha na siasa za kitapeli.  

Ndiyo maana sasa wamechanganyikiwa kuona chama hicho kinakosa mpaka wachangiaji katika harambee zake kama ilivyotokea majuzi jijini Mwanza, kikatumia shilingi milioni 15 kugharamia maandalizi, lakini kikachangiwa shilingi milioni sita tu.

Tayari wimbi kubwa la wanachama, viongozi na wafuasi wa Chadema linazidi kukimbilia CCM baada ya kuchoshwa na siasa za fitina, uzushi, uongo na kila aina ya ghiliba tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2010.

Wanasema waziwazi kuwa “imetosha”, na sasa ‘arobaini’ ya Chadema hatimaye imewadia!

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244


This entry was posted in

One Response so far.

  1. Hakuna mwanaume changudoa kama Charles Charles kihiyo aliyeghushi cheti cha fomu four. Jamaa anaendekeza njaa kujifanya mwandishi wa habari wakati si chochote si lolote bali njaa. Mbona hasemi ukweli kuwa alikuwa mwanachama wa CHADEMA? Kijana huyu mwana haramu asiye na baba anakera Mungu anajua. Charles acha uchangudoa uanze kufikiri kuishi bila kutegemea uongo, kughushi, unafiki na kujikomba kama changudoa.

Leave a Reply