TAARAIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu zangu Waandishi wa Habari Asalam Aleykum.Karibuni katika mkutano huu muhimu wenye lengo la kuzungumzia mustakabali na mwelekeo wa maendeleo ya utoaji wa maoni ya Katiba mpya ijayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Niimelazimika kukutana nanyi haraka kwa nia njema kutokana na matukio yanayojiri yakizidi kutishia amani na utulivu wa kijamii na ukiukwaji wa misingi ya demokrasia kunakofanywa kwa makusudi na chama kimoja cha siasa hapa Zanzibar.
Kumejitokeza vitisho ,vurugu na ghasia za kupanga, kunakoandaliwa na kutekelezwa na wafuasi wa chama hicho cha siasa katika zoezi muhimu linaloendelea la ukusanyaji na utoaji wa maoni mbele ya mikutamno inayoitishwa na makamishna wa Tume ya Rais ya ukusanyaji wa maoni ya Katiba.
Kimsingi vurugu zinazoendelea kutokea katika mikutano hiyo , zimeanza kutia shaka ,kuharibu taaswira nzima na dhana ya mpango huo kwa lengo na madhumuni ya chama hicho kujitafutia umaarufu usiokuwepo ili kuwatia hofu wananchi.
Haya yanayofanyika hivi sasa na kutokea ni matendo maovu,ni uhalifu na zaidi yakitaka kuturudisha tena katika zama nyeusi za mivutano, malumbano na kujenga upya hasama.
Matukio haya kwa sehemu kubwa yana lengo la kuleta mmomonyoko wa kutovumiliana na kutostahamiliana kulikoanza kustawi na hivyo kujenga wasi wasi na hofu iliotoweka baada ya Zanzibar kupoteza maelewano yakutosha tokea mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1992.
Vituko na ghasia hizo zimeanza kuvuruga mwelekeo wa utulivu na amani iliopo tokea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya kumalizika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Chama hicho cha Siasa hakitaki na kinakataa kuheshimu dhana ya mpango huo wa Tume ya Rais unaowataka wananchi wakaazi wa eneo husika kutoa maoni yao , huwa ni mwao kwa mwananchi pale anapotoa maoni yake kinyume na mtazamo wa chama hicho cha siasa.
Ili uonekane bingwa, mwenye uchungu na Zanzibar, mzalendo wa kweli na mwana mageuzi makini,unalazimishwa utoe maoni yanayopendekeza mfumo mpya wa Muungano wa Mkataba na hutakiwi abadan utoe maoni ya Serikali mbili za Kikatiba kama mfumo uliopo hivi sasa.
Mtazamo huo kwa upande mmoja unakabiliwa na nasaba za kihuni, za kipuuzi na kiharamia, zaidi ukikiuka haki za binadamu na demokrasia.
Chama Cha Mapinduzi kinawasihi na kuwaomba wananchi katika maeneo husika ya Mkoa wa Mjini Magharibi waendelee kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao wanayoyaamini bila ya kushurutishwa,kutishwa na kulazimishwa .
Aidha CCM inaitaka Tume ya ukusanyaji wa maoni ya Katiba kulielewa vyema suala hilo na kulichukulia hatua stahiki za haraka kwa mujibu wa sheria husika.
Tunaamini kuwa moni na mawazo ya kila mwananchi kwa ajili ya uundwaji wa Katiba mpya ijayo ni sehemu ya utekelezaji wa misingi ya demokrasia na hapaswi mtu yeyote kuwekewa mipaka au ukomo wa mawazo yake.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
ISSA HAJI USSI GAVU
KATIBU WA KAMATI MAALUM YA NEC
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
ZANZIBAR